Dimba

Omanyala kutifua kivumbi Diamond League ya Shanghai na Rabat baada ya Botswana Grand Prix

Na GEOFFREY ANENE April 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BINGWA wa mbio za mita 100 wa Jumuiya ya Madola, Ferdinand Omanyala ametangaza mashindano saba atashiriki kati ya Aprili 12 na Mei 31 zikiwemo duru tatu za Diamond League.

Afisa huyo wa polisi, ambaye tayari ametimka nchini Afrika Kusini na Uganda mwaka huu, atamenyana na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya Afrika mbio za 100m Akani Simbine kutoka Afrika Kusini kwenye Botswana Golden Grand Prix mjini Gaborone hapo Aprili 12.

Omanyala, ambaye alifuta rekodi ya Afrika ya Simbine katika umbali huo ya sekunde 9.84 akimaliza Kipkeino Classic mwaka 2021 katika nafasi ya pili kwa 9.77, atajitosa katika Diamond League duru ya kwanza mjini Xiamen, Uchina, hapo Aprili 26.

Omanyala akishinda 100m mbele ya Kenneth Bednarek mashindano ya Kipkeino Classic uwanjani Kasarani, Nairobi, mnamo Mei 2023. PICHA | CHRIS OMOLLO

Kutoka Xiamen, bingwa huyo wa zamani wa Afrika ataingia Shanghai Diamond League mnamo Mei 3 na kisha kutimka katika Riadha za Dunia za Kupokezana Vijiti mjini Guangzhou mnamo Mei 10-11.

Mwanaolimpiki huyo kisha ataelekea katika mashindano ya Atlanta City Games nchini Amerika mnamo Mei 17 kabla ya kurejea Afrika kwa duru ya Diamond League ya Rabat nchini Morocco mnamo Mei 25.

Mashabiki watapata fursa ya kushuhudia akifyatuka nyumbani wakati wa Kipkeino Classic Continental Tour mjini Nairobi hapo Mei 31. Alikamata nafasi ya tano kwenye Kipkeino Classic mwaka jana. Atakuwa na presha ya kuandikisha matokeo mazuri kama mwenyeji.

Mashindano makubwa mwaka huu ya riadha za uwanjani ni Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan mwezi Septemba kwa hivyo wanariadha wengi wanajipima na kujipiga msasa kabla ya makala hayo ya 20 kufanyika.