Pep asema timu yake imepata uhai tena
PEP Guardiola, anasema timu yake inayoendelea kurejesha makali yake na inastahili ‘heshima kubwa’ kutokana na ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Bournemouth ugani Etihad jumapili usiku, mechi ya raundi ya 10 Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mshambuliaji matata Erling alichangia mabao mawili katika dakika ya 17 na 33 kabla ya Noco O’Reilly kufunga bao la tatu dakika ya 60. Wageni walipata bao la kufutia machozi dakika ya 25 kupitia kwa Tyler Adams.
Alama hizo tatu ziliipeleka City kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali na alama 19 alama sita nyuma ya vinara Arsenal.
“Nataka kuendelea kuboresha timu hii katika siku zijazo, wiki na miezi ijayo. Naipenda City kwa mambo mengi na natoa heshima kubwa kwa ushindi kwa sababu Bournemouth wako katika fomu nzuri msimu nzuri na hili linaonekana,” aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi.
Aliongezea akisema, “Ikiwa wewe sio mwerevu na unapoteza mipira ovyoovyo, hakuna anayeweza kuwazuia ni timu ambayo wachezaji ni wa kiwango cha juu. Tulijaribu kucheza na pasi nyingi na kupata wakati unaofaa lakini ilikuwa ngumu kwetu kwa sababu wana nguvu nyingi.”
“Natumai Arsenal wanaweza kufungwa bao siku moja. Si rahisi kuwakabili. Ni mechi 10 tu, bado 28 za kucheza. Mambo mengi yatatokea lakini hisia muhimu ni kuwa bora na bora zaidi,” Guardiola alikiri.
Hata hivyo, Halaand alikiri kwamba, “Huu ulikuwa ushindi muhimu. Ni vizuri kurejea baada ya kupoteza mechi muhimu ugenini. Nilijaribu kuchangia kwa timu kwa kufanya kazi yangu na tulishinda tena. Hicho ndicho tunachojaribu kufanya kila wakati. Kwa hivyo sasa tuna mechi mbili muhimu zaidi kabla ya mapumziko ya kimataifa na tuendelee kuzingatia.”
Halaand amecheka na wavu mara 13 katika mechi 10 na anaongoza jedwali la wafungaji bora. Nao Jean Mateta wa Crystal Palace, Igor Thiago wa Brentford, Antoine Semenyo (Bournemounth) na Danny Welbeck (Brighton) wanafuata katika nafsai ya pili wakiwa na mabao sita kila mmoja.
City sasa wanaelekeza macho yote Jumatano hii watakapo menyana na Borussia Dortmund ugani Etihad katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mechi nyingine Jumapili ugani London, West Ham waliwanyorosha Newcastle 3-1.
Katika mechi nyingine Jumapili ugani London, West Ham waliwanyorosha Newcastle 3-1. Mabao ya wenyeji yalifungwa Lucas Paquetá dakika 35′ na Tomás Soucek 97′ nae Sven Botman akajifunga bao dakika ya 50′. Bao la pekee la Necastle lilifungwa na Jacob Murphy dakika ya nne.