Dimba

Sisi ni moto, McCarthy ajinaki Morocco walishindwa cha kufanyia mpira Kasarani

Na CECIL ODONGO August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa Harambee Stars Jumapili  alijinaki kuwa kusoma mchezo na kuwapanga wachezaji wapya kulichangia Kenya kuweka historia kwa kuipiga Morocco 1-0 na kutinga robo fainali ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi ya Nyumbani (CHAN 2024).

Mechi hiyo ambayo ilihudhuriwa na halaiki ya mashabiki kwenye uwanja wa Kasarani ilikuwa ya tatu kwa Kenya tangu mashindano hayo yaanze mnamo Agosti 2.

Licha ya kucheza na wanasoka 10 katika kipindi chote cha pili, Harambee Stars ilionyesha ukakamavu na bidi ya aina yake  ikiweka historia ya kushinda Morocco kwa mara ya kwanza katika mchezo wa soka.

Stars ilichukua uongozi dakika ya 41 baada ya mshambulizi wa Tusker Ryan Ogam kuachilia fataki ambayo ilitinga nyavu na kuamsha uwanja mzima.

Baada ya bao hilo, Kenya ilijipata pabaya huku Chris Erambo akilishwa kadi nyekundu kwa kumkanyaga mchezaji wa Morocco.

Kabla ya kucheza na Kenya, Atlas Lions hawakuwa wamefungwa katika mechi 14 katika kipute cha CHAN.

“Tulikuwa na mbinu ya kujipanga kiasi kwamba Morocco hawakufahamu chochote cha kufanya na mpira. Mechi mbili zikifuatana tukicheza na wanasoka 10, najivunia sana kile ambacho vijana hawa wamefanya,” akasema McCarthy akieleza furaha yake kuhusu ushindi huo.

“Najivunia kama kocha kusimamia vijana hawa. Wakati wa mazoezi nilikuwa naona waliokuwa wamecheza dhidi ya Angola walikuwa wamechoka. Hii ndiyo maana nilifanya mabadiliko hayo na ikiwa ningedumisha timu iliyocheza dhidi ya Angola, tungepata tabu dhidi ya Morocco kwa sababu ya kasi yao,

“Niliwaamini wachezaji niliowaweka hata kama hawakuwa wameanza mechi mbili zilizopita na walijituma sana. Hongera kwetu,” akaongeza McCarthy.

Kwenye kikosi chake, McCarthy alibadilisha beki yake huku Mohammed Siraj, Mike Kibwage na Lewis Bandi wote wakiingia mahala pa Abud Omar, Alphonce Omija na Daniel Sakari ambao walicheza dhidi ya Angola.

Katika safu ya kati, Chrispine Erambo alianzishwa ikizingatiwa Marvin Nabwire alikuwa amelishwa kadi nyekundu dhidi ya Angola. Japo alipewa kadi nyekundu pia, Erambo alikuwa ameonyesha mchezo mzuri na alikuwa injini ya safu ya kati.

“Tulidhibiti mchezo na tukahakikisha kuwa hatari ilipokuwa ikitukodolea macho, tuliiondoa. Nina wingu la matumaini kuwa hatutapata kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Zambia,” akaongeza McCarthy.

Kipa wa Harambee Stars Bryine Omondi alitajwa mchezaji bora wa mechi hiyo kutokana na jinsi alivyowapanga mabeki wake na kuyaokoa makombora ya Morocco.

“Nina fahari sana kushinda Morocco na kupewa tuzo hii ambayo natunuku pia wachezaji wenzangu. Kucheza watu 10 kwenye kipindi cha pili kulikuwa kugumu lakini tumeshinda na sasa lazima tujipange vyema kwa mechi ijayo inayokuja dhidi ya Zambia,” akasema Omondi ambaye alijiunga na Gor Mahia hivi majuzi.

Kutokana na ushindi huo, Harambee Stars inaongoza Kundi A kwa alama saba.

Stars ilishinda Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 1-0 mnamo Agosti 3 kisha Alhamisi iliyopita, walitoka sare ya 1-1 na Angola.

Morocco ina alama tatu baada ya kushinda Angola 2-0 kwenye mchezo wake wa kwanza kisha Angola ina alama moja na ilikuwa ikicheza dhidi ya Zambia ambayo haina alama hapo jana.

Kutokana na ushindi dhidi ya Morocco, Harambee Stars imejizolea Sh42 milioni ambazo zitaenda kwa wachezaji 27 na wanachama 15 wa benchi ya kiufundi.

Kwa kuishinda DR Congo wanasoka hao walilipwa Sh1 milioni kisha Sh500,000 kutokana na sare dhidi ya Angola.

Ahadi hiyo ilitolewa na Rais William Ruto wakati ambapo alitembelea timu hiyo kabla ya kipute cha CHAN 2024 kuanza.

Stars itakuwa ikivaana na Zambia Jumapili hii kwenye mechi ya mwisho ya Kundi A japo tayari wametinga robo fainali. Ushindi kwenye mechi hiyo itahakikisha wanaongoza kundi lao kwa alama 10.

Rais Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga jana waliwaongoza viongozi wa Serikali Jumuishi kupongeza Harambee Stars kwa ushindi huo muhimu.