Suarez anaswa akijaribu tena kuuma mwenzake uwanjani
MWANASOKA mzoefu Luis Suarez, alinaswa na kamera akijaribu tena kumuuma mchezaji uwanjani na akasita tu alipogundua sogora huyo aliyekuwa amemwelekezea meno alikuwa mwenzake katika kikosi cha Inter Miami.
Tukio hilo la kushangaza lilitokea Inter Miami walipokuwa wakimenyana na Los Angeles FC (LAFC) ambao ni watani wao wakuu wa Major League Soccer (MLS) katika mkondo wa pili wa robo-fainali ya Kombe la Mabingwa wa Concacaf wiki jana.
Hali ilitarajiwa kuwa tete jijini Florida baada ya wapinzani wa Inter Miami kushinda mchuano wa mkondo wa kwanza kwa 1-0 jijini California.
Hata hivyo, nyota Lionel Messi na vigogo wenzake walitambisha Inter Miami ambao walisajili ushindi wa 3-1 katika uwanja wao wa nyumbani na hivyo kudengua LAFC kwa jumla ya mabao 3-2.
Hali ya wasiwasi ilitanda uwanjani kuelekea mwisho wa mechi baada ya wachezaji wa pande zote mbili kuanza kuzozana sogora mmoja wa Inter Miami alipokabiliwa visivyo.
Kundi la wachezaji lilijazana katikati ya uga, Suarez akiwemo. Staa huyo wa zamani wa Liverpool na Barcelona alivutwa kwenye ukosi wa jezi yake wakati wa kizaazaa hicho na akazunguka kwa hasira kabla ya kuonekana akilenga kuuma mkono wa mchezaji aliyekuwa akimvuta.
Hata hivyo, alisita kwa haraka baada ya kugundua kuwa mkono huo uliokuwa kwenye ukosi wake ulikuwa wa mchezaji mwenzake wa Inter Miami, Jordi Alba.
Mashabiki walijibu haraka mtandaoni, wa kwanza akisema: “Huo ulikuwa moto wa kirafiki. Alba angeona cha mtema kuni!”
Mwingine aliongeza: “Suarez ni mnyama mbaya. Ana meno makali na hicho ndicho kifaa chake cha ulinzi.”
Mwingine alishauri: “Anahitaji kuona mshauri kuhusiana na tabia hii.”
Ujumbe huo wa mwisho ulihusu historia mbaya ya Suarez ya kuwauma wapinzani kadhaa uwanjani.
Aliwahi kumrarua kwa meno beki Giorgio Chiellini wakati Uruguay iliposhinda Italia 1-0 katika mechi ya Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Ujerumani.
Na mwaka mmoja kabla ya hapo, Suarez alikuwa amemng’ata aliyekuwa difenda wa Chelsea, Branislav Ivanovic, wakati huo akichezea Liverpool.
Hatia hiyo ilifanya Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kumpiga marufuku ya mechi 10 huku kosa la kumng’ata Chiellini likimfanya apigwe marufuku ya mechi tisa za kimataifa kwa kipindi cha miezi 21.