Talaka chungu ya kocha Firat na Kenya serikali ikimlaumu kukosa kufikisha Harambee AFCON
UHUSIANO baina ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) na kocha wa Harambee Stars, Engin Firat umeporomoka baada ya maafisa wapya kuchaguliwa kuongoza soka nchini.
Jana, Desemba 11, 2024, Firat alitangaza kujiuzulu akilalamikia kutolipwa malimbikizi ya mshahara wake ambao duru zinasema unaweza kuwa wa miezi 11.
Rais mpya wa FKF Hussein Mohammed alithibitisha kung’atuka kwa kocha huyo ambaye aliajiriwa Septemba 2021.
Serikali kupitia kwa Wizara ya Michezo ilikuwa imegusia nia yake ya kusitisha majukumu ya kocha huyo baada ya kushindwa kusaidia Harambee Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa Bingwa barani Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco, mwaka ujao.
Mahojiano ya Waziri Kipchumba Murkomen
Katika mahojiano na waandishi wa habari, Jumanne jioni, Waziri wa Michezo, Kipchumba Murkomen alidokeza mwisho wa enzi ya raia huyo wa Uturuki mwenye umri wa miaka 54.
Murkomen aliyezungumza huku akiwa na matuamini makubwa kwa viongozi wapya waliochaguliwa, alimlaumu aliyekuwa rais wa FKF, Nick Mwendwa kwa kumteua Firat, bila kuchunguza vizuri rekodi yake.
“Hata sielewi Firat aliteuliwa vipi kunoa timu ya taifa, kwa sababu hakuna rekodi kamili inayoonyesha ufanisi wake. Kuna wakati nilimuambia Nick machoni mwake kwamba huyo kocha wake wakati mmoja alipigwa 7-0 akiwa na timu ya taifa ya Moldova. Nilijaribu kusoma historia yake na sikuona ufanisi wowote.
“Lakini tulipoingia ofisini tulitulia na kumuunga mkono kikamilifu. Hata kuna wakati alitaka ndege maalum ya kupeleka timu Cameroon na tukampa. Walitaka kuchezea Afrika Kusini, tukagharamia hiyo safari. Lakini baadaye akaanza kusema Stars haikufuzu kwa sababu ilichezea mechi zake katika mataifa ya kigeni! Nilijiuliza kwa nini watu wanashinda mechi za ugenini, ikiwa hiyo ndio sababu?”
Murkomen alisema Serikali itafanya hesabu za Firat na kumlipa kufikia Juni mwaka huu, pamoja na marupurupu mengine kulingana na mkataba wake.
Hussein akisaidiana na Mariga
Alisema ana hakika afisi mpya ya FKF chini ya Hussein Mohamed akisaidiana na McDonald Mariga itatafuta kocha mzuri atakayeongoza timu ya taifa kitaaluma.
“Nimesoma mkataba wake vizuri na nikapata mahali unasema tusipofuzu kwa AFCON 2025 anatakiwa aondoke. Kwa vile hatukufuzu, lazima aheshimu mkataba.”
Baada ya kubanduliwa nje ya Afcon 2025, Firat alieleza nia yake ya kutaka kuendelea kunoa Harambee Stars, lakini baada ya mabadiliko ya uongozi, hali imekuwa ngumu kwake.
Kulingana na mkataba huo, Firat alikuwa akipokea kati ya Sh1.5 na Sh2 milioni kila mwezi, huku kukiwa na madai kwamba hajapokea malipo yoyote kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Firat alipewa jukumu la kunoa Harambee Stars mnamo Oktoba 2020, mechi yake ya kwanza ikiwa dhidi ya Mali ugenini ambapo Stars ilizabwa 5-0 katika pambano hilo la mchujo wa Kombe la Dunia la 2022.
Kusuasua kwa timu hiyo katika mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 pamoja na kushindwa kufuzu kwa Afcon 2025 kulimweka katika hali ngumu.