Dimba

Ten Hag aendea Mourinho ugenini huku akielezea wasiwasi wake

Na MASHIRIKA October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ISTANBUL, UTURUKI

KOCHA Eric Ten Hag ambaye kikosi chake kimekuwa kikisuasua tangu msimu huu uanze ataongoza kikosi chake ugenini Alhamisi usiku dhidi ya Fenerbahce SK ya Jose Mourinho katika mojawapo ya mechi za UEFA Europa League zitakazosakatwa usiku.

Tayari kocha huyo ameeleza wasiwasi wake kutokana na ratiba ya mechi zinazofuata, huku akihofia majeraha zaidi kwa mastaa wake.
Ten Hag amesisitiza kwamba mechi zimefuatana kwa mpigo.

“Licha ya ratiba kuwa ngumu, tunataka kufanya vizuri katika michuano hii ya UEFA Europa League ili tupate tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao 2025/2026,” alisema Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 54.

“Ratiba inatubana, tunalazimika kucheza mechi kila baada ya siku tatu, ni kibarua kigumu kwa wachezaji, lakini itabidi tupambane ili tupate matokeo mazuri ya kutusaidia baadaye,” aliongeza.

United wanarejea uwanjani baada ya mwishoni mwa wiki kuandikisha ushindi wa kwanza katika mechi tano mfululizo.

Mabao ya Alejandro Garnacho na Rasmus Holjund yalikisaidia kikosi hicho kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Brentford katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ushindi katika mechi ya leo utakuwa wa kwanza katika michuano ya UEFA Europa League, baada ya kuokota pointi mbili pekee katika mechi mbili zilizopita dhidi ya FC Twente ya Uholanzi 1-1 ugani Old Trafford na FC Porto ya Ureno 3-3 ugenini.

Haitakuwa kazi rahisi kwa kocha Ten Hag ambaye atakuwa bila mastaa kadhaa wanauguza majeraha.

Luke Shaw na Tyrell Malacia wataendelea kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha mabaya yanayowakabili.

Noussair Mazraouni aliyekuwa akicheza kama beki wa kulia anatatizwa na ugonjwa wa moyo, lakini huenda Diogo Dalot akaendelea kucheza katika nafasi hiyo.

Lisandro Martinez anatarajiwa kucheza kama beki wa kushoto katika nafasi ya Shaw, lakini huenda akaendelea kutatizika kama ilivyokuwa katika mechi za awali.

Kinda Harry Amass ni miongoni mwa wachezaji wachanga wanaotarajiwa kupata nafasi kikosini baada ya kuwa miongoni mwa walioonekana mazoezini Carrighton tangu juma hili lianze.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 hajawahi kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Ten Hag, lakini amekuwa aking’aa katika mechi za vijana.

Tayari, Ten Hag amemtaja kinda huyo kama nyota matata anayeibukia, licha ya umri wake mdogo.

Marcus Rashford anatarajiwa kushirikiana na Garnacho kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imeanza kuamka.

Ratiba ya Europa Alhamisi usiku:
Eintracht vs RFS (7:45pm), AS Roma vs Dynamo Kyiv (7:45pm), Midtjylland vs Union Saint-Gilloise (7:45pm), Qarabag vs Ajax (7:45pm), Tel Aviv vs Real Sociedad (7:45pm), POAK Viktoria Plzen (7:45pm), Fernerbahce vs Manchester United (10pm), Tottenham Hotspur vs AZ Alkmaar (10pm), Lyon vs Besiktas (10pm), Anderlecht vs Ludogorats (10pm).