UEFA: Arsenal waah, Man City wooi!
MANCHESTER, UINGEREZA
SHARTI klabu zinazoshiriki kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya pamoja na Liverpool inayopaa katika Ligi Kuu ya Uingereza zianze kuingiwa na kiwewe kutokana na makali ya Arsenal, wachambuzi wa kandanda barani Ulaya sasa wanasema.
Jarida la standard.co.uk linasema kipigo kikali ambacho Arsenal waliwapokeza wenyeji wake Sporting CP ya Ureno mnamo Jumanne usiku, ni onyo tosha kwa klabu zinazoshiriki mashindano hayo mawili maarufu.
Sporting iliyokuwa chini ya kocha Ruben Amorim aliyehamia Manchester United majuzi, ilikuwa imeitia fedheha Manchester City katika uwanja huo huo wa Estadio Jose Alvade kwa mabao 4-1 mapema mwezi huu.
Huku ikijivunia straika mahiri Victor Gyokeres, matarajio ya wengi yalikuwa kikosi hicho kingetatiza Arsenal nyumbani kwao.
Lakini mambo yalitokea vinginevyo. Vijana wa Mikel Arteta hawakushangaza wengi tu kwa ushindi wa mabao 5-1, bali waliwanyima kabisa wenyeji wao fursa yoyote ya kung’ara. Waingereza waling’aa katika kila idara.
“Pamekuwepo mjadala mkali katika majuma kadhaa yaliyopita kuhusu uwezo wa Arsenal katika kinyang’anyiro cha kushinda taji, lakini sasa ushindi wao mnono dhidi ya Sporting ulidhihirisha uwezo wao mwingi wa kushinda mataji ya Champions League na ligi kuu ya EPL,” likasema jarida hilo.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Gabriel Martinelli kunako dakika ya saba, Kai Havertz (22), Gabriel Magalhaes (45+1), Bukayo Saka (penalti, 65) na Leandro Trossard (82).
Kwa matokeo hayo, Arsenal ilisonga hadi nafasi ya saba katika jedwali la Champions League kwa alama 10 bila kuzingatia matokeo ya mechi za jana usiku. Sporting inafuatia kwa alama hizo hizo 10.
Kwingineko, shida za ulinzi katika kikosi cha Manchester City ziliendelea baada ya kukosa kutulia walipokuwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya Feyenoord kabla ya kutupa mechi hiyo iliyomalizika kwa 3-3 ugani Etihad.
Kutokana na matokeo hayo, City wanashikilia nafasi ya 15 jedwalini, na huenda wakashuka zaidi baada ya mechi nyingine zilizochezwa jana.
Feyenoord inashika nafasi ya 20 kwa alama saba.
Kiungo Ilkay Gundogan, 34, alisema walipoteza mechi hiyo mtindo wa kushangaza. “Sijaamini, kwa sababu tulikuwa tukiongoza zikibakia dakika 15 mechi kumalizika,” alisema Mjerumani huyo.
“Tutajilaumu wenyewe kwa yaliyotokea. Nimekosa majibu kwa maswali mnaoniuliza,” aliongeza.
Kocha Pep Guadiola kwa upande wake alisema wachezaji wake walionekana wadhaifu hasa mechi ikielekea kumalizika.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu watakuwa ugenini Jumapili kucheza na Liverpool katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mechi ambayo Liverpool wanawekewa nafasi kubwa ya kushinda na kuongoza msimamo kwa pengo la pointi 11.
“Sijui kama ni jambo la wachezaji kuchanganyikiwa kiakili, alisema Guardiola huku akionyesha kukatishwa tamaa na utendaji wa upande wake.”
“Tulicheza vizuri wakati tulipokuwa juu kwa 3-0, lakini tukawapa nafasi ya kufunga mabao mengi kwa sababu hatukuwa imara,” aliongeza kocha huyo.
Wakati huo huo, Robert Lewandowski aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu kufunga mabao 100 katika kabumbu hii alipoongoza Barcelona kuibamiza Brest 3-0 ugani Camp Nou.
Cristiano Ronaldo ndiye anayeongoza kwa ufungaji mabao katika mashindano haya ya Ulaya baada ya kucheka na nyavu mara 141 akifuantwa na Lionel Messi.
Jijini Barcelona bao la Lewandowski lilipatikana kupitia kwa mkwaju wa peanlti. Ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Brest umwawezesha kusonga hadi nafasi ya pili jedalini baada ya kushinda nne kati ya mechi tano, wakati Brest walishuka hadi nafasi ya nane kwenye msimamo huo unaojumuisha timu 36.
Kwingineko, Inter Milan waliandikisha ushindi wanne mfulilizo kwenye michuano hiyo baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya RB Leipzig ugani San Siro.
Kabla ya mechi za jana, vijana hao wa kocha Simone Inzaghi walikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo. Bao la ushindi lilifungwa na Castello Lukeba aliyefunga langoni mwake akijaribu kuokoa fri-kiki ya Federico Dimarco dakika ya 27.
Kwenye mechi nyingine iliyochezewa Wankdorf, Atalanta waliendeleza rekodi yao ya kutofungwa walipowakung’uta Young Boys 6-0. Charles de Ketelaere alifunga mabao mawili huku mengine yakipatikana kupitia kwa Mateo Retegui, Sead Kolasinac na Lazar Samardzic, wakati Bayern Leverkusen wakiandikisha ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya Red Bull Salzburg.
Matokeo ya mechi za Jumanne yalikuwa:
Sporting Lisbon 1 Arsenal 5, Young Boys 1 Atalanta 6, Barcelona 3 Brest 0, Leverkusen 5 RB Salzburg 0, Inter Milan 1 RB Leipzig 0, Bayern Munich 1 PSG 0.