Upangaji mechi: Vuguvugu lataka wasaliti wa taifa wachukuliwe hatua kali
RAIS wa vuguvugu la Bunge la Mwananchi, Francis Awino, amelaani vikali vitendo vya hongo katika soka ya Kenya hasa vinavyohusu timu ya taifa ya Harambee Stars.
Katika mahojiano na Taifa Leo hapo Jumamosi rais huyo alitaja madai yanayohusu kipa Patrick Matasi kupanga matokeo ya mechi kabla ichezwe kama kitu kinachosikitisha sana.
“Soka ni mchezo wa hisia kali, fahari na kuunganisha taifa. Mchezaji anapoingilia vitu visivyo na maadili mema na vinavyotia doa uadilifu wa mchezo huu, hiyo sio tu kusaliti wachezaji wenzake, bali taifa nzima,” akasema Awino.
Ameongeza kuwa matendo kama hayo yanaharibia vijana walio na talanta maisha ya usoni, yanazuia uwekezaji katika soka na pia yanachafulia Kenya jina kimataifa.
“Naomba asasi zenye uwezo wa kisheria ikiwemo Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na idara za kijasusi kuchunguza kwa kina tukio hilo. Yeyote atapatikana na hatia achukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe funzo kwa wengine wanaoweza kushawishiwa kutumbukia katika ufisadi kama huo,”
Kama Bunge la Mwananchi, afisa huyo alisema kuwa “tunasimama upande wa haki, uwajibikaji na matendo ya haki”.
“Soka ya Kenya lazima ilindwe dhidi ya visa vya ufisadi. Tushirikiane kuhakikisha michezo yetu inasalia safi, ina utaalamu na inafaidi talanta nyingi changa zinazojitahidi kuinuka na kuweka Kenya juu kwenye ramani ya dunia,” akahitimisha.
Matasi amejipata pabaya pamoja na kupigwa marufuku na FKF siku 90 baada ya video kuenea mitandaoni kuwa mtu anayedaiwa kuonekana akipanga matokeo ya mechi kwenye video hiyo ni yeye.
Kipa huyo nambari moja wa zamani wa Harambee Stars amekana madai hayo.
Si mara ya kwanza Matasi anatuhumiwa kwa kushiriki upangaji mechi katika kiwango cha klabu au timu ya taifa. Alilaumiwa sana na Wakenya wakati Harambee Stars ilipepetwa 4-1 na Cameroon mechi ya mkondo wa kwanza ya Kundi J kufuzu kwa Kombe la Afrika 2025. Mchuano huo ulisakatiwa uwanja wa Ahmadou Ahidjo, Yaounde.