Buda mkali taabani baada ya kufumaniwa kwa jirani akimega asali ya pembeni
VIPUSA wa boma la hapa walishangilia mjomba wao mkali alipojiharibia jina ilipojulikana ana mpango wa kando.
Kulingana na duru, buda huyo ni mkali sana na mara kwa mara huwasuta wanadada wa boma hilo kwa sababu ya vituko vyao.
Isitoshe, inasemekana mara kadhaa mzee hakujizuia kuwatandika warembo kwa kuchafua jina la familia.
“Juzi, ilikuwa mguu niponye kwa buda huyo alipofumaniwa akiramba asali kwa jirani na akaponea chupuchupu kupewa kichapo cha mbwa,” mdaku akaeleza.
Warembo walipopata habari waliangua kicheko wakisema mjomba wao hatakuwa na ujasiri wa kuwakosoa kwa sababu alijikosea heshima.
Lakini mama zao wakawaonya kuwa watajipata taabani wakizidisha tabia mbaya.