Demu atema mume aliyejaribu kuzima nyota yake ya kwenda ng’ambo
MWANADADA aliamua kumtema mume wake alipomkataza kusafiri nchini Amerika alikopata kazi ya mshahara mnono katika shirika moja la kimataifa.
Wawili hao wamekuwa wakiishi hapa mjini Msambweni, Kaunti ya Kwale, wakipambana na maisha bila mapato ya kuridhisha.
Kila mmoja alikuwa akisaka kazi na juzi na bahati ilibisha wakati demu alipata kazi na shirika la kimataifa.
Shirika hilo likamtuma kwanza ng’ambo kule Amerika kwa miezi sita kabla kurejea kufanya kazi nchini.
Hata hivyo, jamaa hakuchangamkia bahati ya mkewe na akamkataza kwenda safari hiyo.
Kauli yake ilimkasirisha mwanadada na juhudi za kumshawishi mumewe zilipogonga mwamba aliamua kumtema, na kujulisha wazazi wa pande zote mbili sababu za kufanya hivyo.
Polo alipapurwa vikali na wazazi wake kwa kujaribu kuzima nyota ya mkewe.