Dondoo

Demu awakia mpenziwe kwa ahadi hewa ya kumlipia ‘rent’

Na JANET KAVUNGA October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

CHANGAMWE, MOMBASA

DEMU mmoja alizua kisanga mtaani hapa baada ya kumkabili mpenzi wake hadharani, akimtaka aache kumchukulia kama mjinga kwa kumpa ahadi za uongo.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, kipusa huyo alifika ghafla na kumvamia jamaa aliyekuwa akisubiri basi huku akitabasamu, akamvuta kando na kuanza kumwaga hasira.

“Uliahidi utanisaidia kodi ya nyumba na hadi leo umekuwa ukinipiga tu hadithi. Usidhani kwa sababu nakunyamazia basi mimi ni mjinga,” alisikika akisema kwa sauti.

Jamaa alijaribu kuongea lakini kipusa hakumpa nafasi.

“Nimevumilia vya kutosha. Mwanamume wa kweli hutimiza ahadi, si porojo kila siku. Kama huna nia, niambie mapema!”

Watu walikusanyika kushuhudia drama hiyo iliyomalizika kwa kipusa kuondoka kwa hasira huku jamaa akibaki mdomo wazi.