Dondoo

Deni lasimamisha harusi ghafla

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

SOSIET, KERICHO ?

Siku iliyotarajiwa kuwa ya furaha tele iligeuka kuwa yenye huzuni nyingi mzee alipositisha harusi ya binti yake kwa sababu ya deni.

Inasemekana baba ya kipusa alimuamrisha pasta kusimamisha harusi ya binti yake akidai baba ya jamaa alikuwa adui yake.

Duru zinaarifu kwamba hapo awali, wazee hao wawili walikuwa marafiki wa chanda na pete. Uhusiano baina yao ulidhoofika baba ya jamaa alipokataa kumlipa baba ya kipusa hela alizokuwa amemkopa.

Inasemekana watoto hawakuwa wakijua uhasama uliokuwepo baina ya wazazi wao. Wao waliendelea kulipalilia penzi lao hadi siku ya harusi ilipofika.

Duru zinasema tukio hili likifanyika, kanisa lilikuwa limejaa kupindukia.

“Pasta, nakuomba kitu kimoja. Bwana na Bi harusi wasivishane pete kwanza. Kuna kitu hakiniridhishi,” baba ya kipusa alisema.

Watu walitega masikio kupata habari za mzee huyo. “Hakuna vile binti yangu ataolewa katika boma la hasidi wangu. Haiwezekani,” mzee aliapa. ?Pasta alimuomba mzee aelezee zaidi.

“Baba ya kijana huyu ana deni langu kubwa sana. Hata mahari aliyoleta haiwezi kulipa hilo deni. Kila mara yeye hunizungusha tu. Juzi tulipopatana barabarani alinitusi vibaya sana,” mzeee alidai.

Pasta alimuomba mzee aruhusu harusi iendelee ili mambo mengine yasuluhishwe baadaye lakini hakutoboa.

“Msichana wangu ninarudi naye nyumbani. Vijana wa kutafuta wake wa kuoa ni wengi. Atapata mwingine,” mzee alifoka.

Penyenye zinasema baba ya jamaa alijaribu kuomba msamaha lakini msamaha wake uligonga mwamba.

“Acha kujifanya. Kila mtu anakujua kama mzee uliyejaa matusi. Hata mahari ya mwanao sijaitumia. Mje mkachukue,” mzee alimfokea babake bwana harusi. Pasta hakuwa na jingine ila kusitisha harusi.