Jombi azimia kung'amua mke ana mwanaharamu
NA NICHOLAS CHERUIYOT
BELGUT, KERICHO
Jombi wa hapa, alizimia kwa muda baada ya kugundua kuwa mkewe ana mtoto wa kiume aliyezaa kabla ya kuoana.
Inaarifiwa kuwa jamaa na mkewe walioana miaka kumi iliyopita na wamekuwa na maisha ya ndoa ya furaha.
Siku ya tukio, jamaa alikuwa akitangatanga mtaani alipopigiwa simu na shemeji yake mmoja.
Baada ya salamu za kawaida, jamaa aliambiwa ajitayarishe kwa sherehe ya kabla na baada ya jandoni kwa mwanawe.
“Alishauriwa kuwa atagharimia kila kitu lakini sherehe itafanyika kwa wakwe zake,” mdaku aarifu.
Jamaa alicheka akidai kuwa aliyempigia simu alikuwa amekosea nambari lakini akaelezwa kwa kina vile mkewe alivyozaa akiwa bado katika shule ya sekondari.
Alifahamishwa polepole kuwa baba ya kijana huyo hajulikani na kwa hivyo sharti awajibike kama baba kwa kuwa alimuoa mama yake.
Ufichuzi huo ulimchoma jombi sana na akafululiza hadi kwake kumdadisi mkewe.
“Kumbe tayari ulikuwa mzazi wakati tukichumbiana? Ndoa hii itaporomoka leo nikijua kuwa yale niliambiwa ni ukweli,” jamaa alinguruma huku akitetemeka kwa hasira.
“Mrembo alivamiwa na wasiwasi na kusitasita kabla ya kuongea vizuri,” mdaku aarifu.
“Naomba msamaha kwa kuficha habari ya mwanangu wa kiume. Hata nilikuwa na mpango wa kukuelezea. Hata hivyo, usiwe na shaka maana sitakutwika jukumu la kumlea au kumlipia karo. Nimejipanga na hutatoa hata senti,” mrembo alisema kwa ukakamavu.
Inaelezwa kuwa ufichuzi ulikuwa mzito kwa jombi na akazirai. Ilikuwa afueni kwa jamaa zake polo aliporudiwa na fahamu upesi na akaanza kupatiwa ushauri moja kwa moja.