Kalameni ajigamba atapiga ‘mechi’ kali punde baada ya kuachiliwa kortini
MWANAUME aliyeachiliwa huru Nairobi, Januari 20, 2026 baada ya kesi iliyomkabiliu kutupiliwa mbali alishangaza kila mtu kortini alipotangaza wazi wazi, “leo nitapiga ‘mechi’ sawa sawa nishukuru Mungu na pia nisherehekee kufutiliwa makosa.”
Huku akipiga makofi na kutabasamu akiangua kicheko na kuanika meno alisema “leo nitajitolea sawa sawa nifunge mabao, kwa muda mrefu nimekuwa siko katika hali ya kuchangamkia mambo.”
Akihojiwa na mwandishi wetu, baba huyo mwenye umri wa miaka 35 alisema alisusia tendo la ndoa kwa vile hakuwa anajua kesi ingeendaje.
“Kwa hakika ukishtakiwa hujui mwisho wa kesi utakuwa aje. Nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda nikatoswa gerezani na kuacha mke wangu mpendwa bila mtu wa kumtunza na kumjulia hali. Lakini sasa mambo ni bam bam. Nimeachiliwa na njia ya kujitangaza nipo ni ‘mechi’. Mama jiandae naja,” baba huyo kutoka magharibi mwa Kenya alitangaza hadharani.
Mwanaume huyo alikuwa ameshtakiwa kuchochea vurugu na vurumai kutokana na msimamo wake kisiasa.