Kioja majoka kumkabili polo akiiba mazao shambani
Na CORNELIUS MUTISYA
NDIVU, MACHAKOS
POLO wa hapa, nusura ateguke guu akikimbilia usalama wake alipovamiwa na kundi la majoka muda mfupi baada ya kuingia katika shamba la mwenyewe kuiba matunda.
Kulingana na mdaku wetu, polo alikuwa akifanya biashara ya kununua na kuuza matunda aina ya ‘passion’ mjini Machakos na vitongoji vyake. Bidii yake ya mchwa katika biashara hiyo ilimfanya kipenzi cha wengi.
“Polo alipendwa sana. Hata alibandikwa jina la msimbo ‘mtu wa passion’ kutokana na biashara yake,’’ alisema mdokezi.
Inasemekana kwamba, matunda hayo yalianza kuadimika mashambani kutokana na kiangazi kilichokithiri eneo hili na biashara ya polo ikaathirika mno.
Alikuwa akimaliza hata miezi miwili bila kupata matunda ya kuwauzia wateja wake.
Hata hivyo, alipokuwa katika pilkapilka za kikazi mtaani, kwa upeo wa macho yake aliona shamba moja lililojaa matunda hayo na akayatamani. Aliuliza wapita njia mwenye shamba hilo na wakamwambia alikuwa amesafiri.
“Polo aliuliza aliyekuwa akimiliki shamba hilo na alipofahamishwa kwamba alikuwa safarini aliamua kuvuna asikopanda,’’ alisema mdokezi.
Twaarifiwa kwamba, tamaa ya kupata pesa za haraka ilimwingia polo na akaamua kuingia katika shamba hilo avune matunda ya mwenyewe bila idhini!
Hata hivyo, wakati alipokuwa akikopoa tunda la kwanza, majoka manne yalijitokeza ghafla na kuanza kumshambulia. Kulingana na mdokezi, jamaa alitoka shoti kabla hayajamdhuru na akatokomea huku akipiga nduru.
“Watu wa siku hizi wamechanuka mno. Wamejua mbinu muafaka za kulinda mali yao!’’ alisema jamaa mmoja aliyeshuhudia kioja hicho cha saa tisa alasiri.