Dondoo

Kipusa agawa asali kulipiza kisasi

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Tobbie Wekesa

KABUCHAI, BUNGOMA

POLO mmoja wa eneo hili, alishindwa kujieleza alipogundua kuwa mkewe alitekeleza tishio lake la kugawa asali.

Inasemekana kipusa alikuwa ametishia kuchepuka iwapo polo asingekoma kuwa na mipango ya kando.

Kulingana na mdokezi, kipusa alikuwa amekasirishwa na tabia ya jamaa ya kutongoza wanawake wa wenyewe.

Inadaiwa kipusa alijaribu kumkanya polo aachane na tabia hiyo lakini hakukoma.

Inasemekana mara kwa mara wawili hawa walikuwa wakigombana.

Kulingana na mdokezi, kipusa alipoona polo hakuwa tayari kuacha tabia hiyo, naye aliamua kufuata njia hiyo hiyo.

“Usifikirie mimi ni jiwe. Wazungu walisema ‘you do me, I do you’. Sitaki kusikia ukilalamika,” kipusa alimfokea polo.

Penyenye zinasema polo alianza kumzomea kipusa lakini mwanadada alikuwa ameamua.

Juzi jamaa aligundua kuwa kipusa alikuwa ameanza kutekeleza tishio lake.

Inadaiwa polo aliondoka asubuhi na aliporejea jioni, hakumpata mkewe. Alipojaribu kumpigia simu, kipusa hakupokea ila alimtumia ujumbe kumuarifu ajipange.

Inasemekana polo alibaki mdomo wazi. Kipusa aliporejea, alimkuta polo kwenye kochi.

“Mbona leo umerudi mapema hivi? Ama hukuwa na mteja?” kipusa alimuuliza polo.

Duru zinasema polo alipomuuliza kipusa alikotoka, jibu la kipusa karibu limpe polo mshtuko wa moyo.

“Tangu tuoane hatujapata mtoto. Shida ni wewe. Unalima mashamba mengi kisha ukirudi kwangu huwa umechoka. Acha nitafute vijana barobaro huko nje wanaoweza hii kazi,” kipusa alimfokea polo.

“Shughulikia hali yako nami nishughulikie yangu. Ukifanya nami nafanya. Ukirudi kwa nyumba hata nami narudi. Kwani kuna nini,” kipusa aliuliza.

“Ukitembelea vimada wako, nami natembelea wangu. Tuwe sambamba,” mwanadada alieleza bila kupesa jicho.