Kisura taabani kumtandika mumewe kila siku
Na TOBBIE WEKESA
Tulienge, Bungoma
Kipusa mmoja wa eneo hili alijipata pabaya baada ya wazee wa ukoo kumuonya vikali dhidi ya kumuadhibu mume wake.
Inasemekana kipusa alikuwa na mazoea ya kumpa kichapo kila mara akifika nyumbani kwake hadi wazee wakaamua kumuita kikaoni na kumpa onyo.
“Wewe unatuaibisha na ukoo kwa jumla. Kila mara ni kumchapa mumeo. Shida yako ni gani?” wazee walimuuliza mwanadada. Kipusa alidai kwamba hakuwa na shida yoyote na kudai kwamba mumewe ndiye hajakomaa kiakili. “Huyu kijana wenu nikimuachilia awe huru, atapotoka,”mwanadada alijitetea.
Penyenye zinasema kipusa alikuwa amempa polo masharti makali mno. Mojawapo saa moja ya jioni isimpate nje ya boma.
“Tunajua una nguvu nyingi sana. Hufai kumalizia hizo nguvu zako kwa kijana wetu. Nenda ukawe mwanandondi,” mzee mmoja alimwambia kipusa.
Inadaiwa kipusa aliapa kuendelea kumuadhibu polo iwapo hatabadili tabia na mienendo yake.? “Wewe huoni aibu mwanamume mzima kulia kama mtoto mdogo! Hilo lazima likome. Hili linafanya ukoo na familia hii kusemwasemwa sana kule nje,” kipusa alionywa.
Kipusa alilazimika kunyamaza alipoona wazee wote waliungana dhidi yake. ?“Siku mbili haziwezi kupita kama bwanako hajasikika akilia. Sisi hatutakubali kubandikwa majina ya dharau kwa sababu yako,” wazee walimuonya kipusa.
Kulingana na mdokezi, hata majirani hawakufurahishwa na namna kipusa alivyokuwa akimuadhibu mumewe. Kwao, kipusa alikuwa akitoa mfano mbaya kwa wanawake wenzake na wasichana wadogo.
Duru zinasema wazee hao walimlazimisha kipusa kuomba msamaha na kuahidi kutorudia tena tendo hilo.