Nusura avishwe tairi kwa kuchungulia wanandoa wakilishana asali
Na LUDOVICK MBOGHOLI
Kasarani, Mombasa
Kalameni mmoja mtaani hapa nusura ateketezwe na wanakijiji walioshuku kwamba alikuwa mwizi walipompata akichungulia wanandoa wakirushana roho katika nyumba yao.
Yasemekana jamaa alikuwa na tabia ya kuchungulia madirishani usiku wa manane kuangalia yanayofanyika kwenye nyumba za watu.
“Jamaa alikuwa na mazoea ya kuchungulia watu hasa wanaume na wake wao wakirushana roho vitandani na juzi alichungulia dirisha la jirani mambo yalipomwendea mrama,” alisema mdokezi.
Penyenye zinasema kwamba jirani aliona pazia ikisukumwa upande mmoja ndipo akapiga nduru akidhani alikuwa amevamiwa na wezi.
Inasemekana kwamba majirani waliamka na kutoka nje na kumfumania jamaa akiendelea kupiga chabo bila woga.
Mdaku anaelezea majirani walimuuliza alikuwa akifanya nini, naye akatimka mbio lakini kelele za watu wakidai alikuwa mwizi zilipasua anga na kualika wapita njia waliomfukuza na kumkamata wakitaka kumwadhibu.
“Wapita njia tayari walichukua petroli na tairi wakinuia kumteketeza lakini kabla ya adhabu ya kifo kumpata alilalamika akisema alikuwa akichungulia tu dirishani lakini hakuwa na nia ya kuiba,” alieleza mdokezi.
Mdokezi anasema majirani walimtambua lakini wakadai lazima wamfunze adabu ili aache tabia ya kupiga chabo usiku kuwachungulia madirishani.
“Umezoea vibaya, leo hatukuachi, tutakufunza adabu ujue ni vibaya kuchungulia watu wakiwa makwao,” jirani mmoja alimweleza jamaa.
Kwa mujibu wa mdokezi, jamaa alipokezwa kichapo cha haja hadi akatubu.
“Alisema hatarudia tabia hiyo tena. Aliapa kwa jina la mwenyezi Mungu na kuomba msamaha,” alisema mdokezi.
Majirani walimuacha na kumuonya vikali kisha wakamwambia ajipeleke hospitali kutafuta matibabu.