Dondoo

Polo aachwa mapengo alipogonga mlingoti wa mulika mwizi akizubaia kidosho

Na SAMUEL MUIGAI August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JOGOO ROAD, NAIROBI

ILIBIDI kalameni mmoja atafute huduma za dharura za matibabu alipong’olewa meno kadhaa na mlingoti wa taa ya kuangaza mtaani, maarufu mulika mwizi, wakati alipinduka kufuatiliza macho kwa kidosho waliyekutana njiani.

Polo huyo anayefahamika kwa kubadilisha warembo kama soksi alikuwa njiani kuelekea katika uwanja mmoja mtaani ili kushangilia timu yake ya soka, alipokutana na kidosho aliyemzuzua. 

Jamaa alipomuona alitaka kumsalimia lakini akanywea kidogo. Wakati akisuka maneno matamu akilini ya kuporomosha, naye demu alizidi kumkaribia hadi wakapitana.

Polo alipendua shingo akamfuatilia kidosho kwa macho akisononeka nyara imempita, badala ya kuzingatia mbele anakoenda.

Maskini hakuona mlingoti wa mulika mwizi uliokuwa mbele yake, akaulima pah! Damu ikaanza kumtiririka na meno kadhaa yakang’oka papo hapo.

Aibu ilimfanya kuvumilia uchungu huo kwani hakupiga duru asitake kuonyesha kidosho kuwa ameumia. Akakaza kiguu na njia kutafuta kliniki ya kumpa matibabu ya dharura kuokoa kinywa chake.