Polo aponea kifo alipofumaniwa ‘akitafuna mbuzi’ katika zizi la jirani
Na TOBBIE WEKESA
KWAMWENJAS, NYERI
KALAMENI mmoja aliponea kwenye tundu la sindano alipofumaniwa na mzee wa boma akiwa katika chumba cha binti yake.
Kulingana na mdokezi, baba ya mrembo alikuwa akitoka kwa boma la jirani. Alipofika kwa boma lake, aliamua kupitia karibu na chumba cha binti yake ambapo alishtuka kusikia sauti nzito kutoka ndani.
Mzee aliamua kusimama ili kubaini sauti ilikuwa ya nani na nini kilichokuwa kikiendelea ndani. “Hii sauti haikosi ni ya mwanaume. Leo atanijua,” mzee aliapa.
Inadaiwa polo alikuwa amemtembelea mrembo na kisha akaalikwa chumbani kisiri. Duru zinaarifu kwamba chumbani, polo alikuwa tayari juu ya mzinga akirina asali. Kilichomuuza ni sauti yake nzito.
Habari zilizotufikia zinasema mzee aliamua kuugonga mlango kwa mkongojo aliokuwa ameshika. “Hiyo sauti ni ya nani?” mzee alimuuliza binti yake.
Binti hakumjibu mzee. “Nauliza ni nani huyo yuko humu ndani? Nataka kumjua,” mzee alizidi kuteta.
Inadaiwa kuwa mzee alianza kuusukuma mlango akitaka kuingia ndani kwa nguvu. “Mnafanya nini humu ndani?” mzee aliwakaripia. Kwa kugundua kuwa chuma chake ki motoni, polo alianza kutafuta namna ya kuhepa.
“Hauna aibu kuja kwangu bila idhini. Leo mtu lazima mguu ubakie hapa,” mzee aliapa huku akiwaita majirani.
Penyenye zinasema polo alijipenyeza kwenye dirisha na kutimua mbio kabla ya majirani kufika.
“Kijana wewe una bahati. Hiyo sauti yako peleka mbali kabisa. Huwezi kuja na kula katika zizi langu. Nikikupata tena utajua mimi ndiye mwenye hii boma,” mzee alimkemea polo huku akimfuata nyuma.