Yambidi atoroke ukweli wa mimba usijulikane
Na TOBBIE WEKESA
Mathare, Nairobi
Kipusa aliyekuwa akiishi katika ploti moja mtaani hapa aliwashangaza marafiki zake alipofunganya virago na kuhamia mtaa mwingine akihofia kujifungua mtoto anayefanana na mpango wake wa kando.
Kulingana na mdokezi, kipusa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kalameni fulani ambaye walikuwa wakiishi ploti moja.
Inasemekana jamaa huyo alikuwa na familia lakini ilikuwa ikiishi mashambani.
Duru zinaarifu kwamba familia ya jamaa ilimtembelea na kipusa alishangaa kuona kwamba watoto wote walikuwa wakimfanana na polo.
Jambo hili lilimtia kipusa wasiwasi akihofia hata mtoto atakayejifungua huenda akafanana na jamaa.
Kipusa aliamua kutulia kidogo akifikiri familia ya jamaa ingerudi mashambani. Juma moja lilipita, hakuna lolote lililofanyika. Mwezi ukapita na hawakuondoka.
Baada ya miezi mitatu, kipusa akikaribia kujifungua, familia ya jamaa ilikuwa haionyeshi dalili za kuondoka. Duru zinasema kipusa alihofia sana siri zake zingejulikana na wapangaji wa ploti hasa mumewe kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba mimba aliyokuwa amebeba ilikuwa ya mpango wake wa kando.
Habari zilizotufikia zinadai kwamba uhusiano wa kipusa na polo ulikuwa ukiendeshwa kwa siri kubwa mno.
“Hata mume wa kipusa siku zote aliamini kwamba mimba aliyokuwa amebeba mkewe ilikuwa yake. Hakufikiri mkewe angeweza kuwa na mpango wa kando,” alieleza mdokezi.
Ilimbidi kipusa amshawishi mumewe wahamia ploti nyingine.
“Kwani kuna nini hicho kinachokufanya useme tuhame? Tumeishi nawe hapa kwa zaidi ya miaka mitatu. Mbona wahama?” kipusa aliulizwa na rafiki yake.
Kipusa alimueleza kwamba alitaka kuhamia kwingine kwani alikuwa amechoshwa na kuishi hapo na alitaka kujifungua katika mazingira mapya.