Habari za Kitaifa

Duale ashtakiwa kwa madai ya kukosa kusitisha uvunaji changarawe

Na KITAVI MUTUA September 7th, 2024 1 min read

WAKAZI wa eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui, wamemshtaki Waziri wa Mazingira Aden Duale na mashirika kadhaa ya serikali kwa madai ya kukosa kusitisha uzoaji wa changarawe ambao umesababisha uharibifu mkubwa wa kimazingira.

Bw Duale anashtakiwa pamoja na Serikali ya Kaunti ya Kitui, Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA), Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (Nema) na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kitui na Kamishna wa Kaunti kwa kushindwa kwao kutekeleza sheria zilizopo ili kulinda mito.

Kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi huko Kitui na wakulima wadogo 158 wa Mwingi, tayari imeidhinishwa kuwa ya dharura na itasikilizwa wiki ijayo.

Wakazi hao wamedai kuwa kila mmoja kati ya wahusika kumi na moja katika kesi hiyo, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kukomesha uchimbaji kiholela na uzoaji haramu wa changarawe kutoka mito ya msimu iliyo karibu ambayo ni tegemeo lao pekee la maisha.

Walalamishi wanadai uchimbaji haramu wa changarawe umeathiri vibaya mazingira yao.

Wametoa orodha ya malori 58 yaliyopigwa picha yakibeba changarawe katika vijiji na wanaomba agizo la kudumu la mahakama kuwazuia washtakiwa kuendelea kuruhusu au kujihusisha na uchimbaji na uzoaji wa changarawe.

Wakazi hao ambao wanaowakilishwa mahakamani na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Kenya Eric Mutua, wanadai kuwa kama Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Bw Duale ameshindwa katika jukumu lake la kuongoza utekelezaji bora wa sera ya kitaifa na usimamizi wa uhifadhi, ulinzi na usimamizi wa mazingira.

Serikali ya Kaunti ya Kitui imelaumiwa kwa kushindwa kutekeleza sheria maalum ya Utumiaji na Uhifadhi wa Changarawe katika Mabonde ya Mto ya Kitui, ambayo ilipitishwa kuzuia uzoaji haramu wa changarawe.

Licha ya Mahakama Kuu kuwa katika likizo yake ya kila mwaka, Jaji Lilian Kimani wa mahakama ya Mazingira ameidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kupanga kusikilizwa kwa njia ya mtandao Septemba 12, 2024.