Michezo

Eliud Kipchoge asema yuko tayari kutetea ubingwa wa London Marathon

Na GEOFFREY ANENE October 1st, 2020 2 min read

“NAHISI niko sawa kabisa na ninafurahia kurejea hapa.” Huo ndio ujumbe kutoka kwa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 ya wanaume Eliud Kipchoge akiwa nchini Uingereza akijiandaa kutetea taji lake la London Marathon hapo Oktoba 4, 2020.

Akizungumza na wanahabari hapo Jumatano, Kipchoge, 35, aliongeza, “Nadhani mbio zitakuwa za kufana hapo Jumapili. Naomba mashabiki wote washiriki mbio hizi popote waliko, wazikamilishe na kuzifurahia. Tuko pamoja kiroho. Pamoja tunaweza kudhibiti ugonjwa wa covid-19.”

Mkimbiaji huyo aliyeweka rekodi ya dunia ya kilomita 42 ya saa 2:01:39 kwenye mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2018 atakuwa akitafuta ubingwa wa London Marathon kwa mara yake ya tano baada ya kubeba mataji ya mwaka 2015, 2016, 2018 na 2019.

Bingwa huyo wa Olimpiki anashikilia rekodi ya London Marathon ya saa 2:02:37 aliyoweka mwaka 2019.

Atakabiliwa na kibarua kigumu kuhifadhi taji lake linalomezewa mate na Muethiopia Kenenisa Bekele, ambaye alikosa rekodi ya dunia ya Kipchoge kwa sekunde mbili pekee aliposhinda Berlin Marathon kwa saa 2:01:41 mwaka 2019.

Bekele amewahi kushiriki London Marathon mara tatu. Alikamilisha makala ya mwaka 2016 katika nafasi ya tatu, zaidi ya dakika tatu nyuma ya Kipchoge alitawala kwa saa 2:03:05, huku Mkenya mwingine Stanley Biwott akikamilisha wa pili (2:03:51).

Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 38 aliimarika mjini London mwaka 2017 alipomaliza katika nafasi ya pili kwa saa 2:05:57, sekunde 0.09 nyuma ya mshindi kutoka Kenya, Daniel Wanjiru. Mara ya mwisho Bekele alishiriki London Marathon ilikuwa mwaka 2018 aliporushwa hadi nafasi ya sita akikamilisha kwa saa 2:08:53 nyuma ya Kipchoge (2:04:17), Muethiopia Shura Kitata (2:04:49), Muingereza Mo Farah (2:06:21) na Wakenya Abel Kirui (2:07:07) na Bedan Karoki (2:08:34) waliofuatana katika nafasi tano za kwanza katika usanjari huo. Mzawa wa Mogadishu nchini Somalia, Farah yuko katika orodha ya wawekaji kasi jijini London hapo Jumapili.

Aidha, Kipchoge, ambaye atafikisha umri wa miaka 36 hapo Novemba 5, ameomba wanariadha kuja Kenya kufanyia mazoezi yao. “Naomba wanariadha wote na watu kutoka dunia nzima waje Kenya na kufanyia mazoezi yao. Serikali imeweka mikakati bora ya kuwahakikishia usalama wenu,” alisema Balozi huyo wa kunadi Kenya kwa watalii.

Mazoezi ya maeneo ya juu yamepata umaarufu na mji wa Iten ni moja ya sehemu inayopendwa na wanariadha kufanyia mazoezi yao. Maeneo mengine nchini Kenya yanayopendwa na wanariadha ni Ngong, Kaptagat, Kapsabet na Longonot.