Makala

Elizabeth Nyokabi: Mwalimu pekee wa kike anayefunza watoto msituni Boni licha ya vitisho vya Shabaab

Na KALUME KAZUNGU July 30th, 2024 3 min read

ELIZABETH Nyokabi Njogu, 38, ni mja aliyejitolea kwa hali na mali ilmuradi aifikishe elimu kwa jamii ya wachache ya Waboni wanaoishi ndani ya msitu mkuu wa Boni, Kaunti ya Lamu.

Sifa za Msitu wa Boni miaka nenda miaka rudi katu hazijakuwa nzuri kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab. Ni eneo ambalo kwa muda mrefu limevuta mkia karibu kila sekta, iwe ni elimu, miundomsingi kama barabara, afya na kadhalika.

Mnamo 2014, vijiji vya msitu wa Boni viligubikwa na wingu jeusi pale shule tano na zahanati zote zilizokuwa zikihudumu eneo hilo zilipofungwa ghafla kutokana na mashambulio ya mara kwa mara ya Al-Shabaab.

Walimu, madaktari na wauguzi waliohudumia shule na vituo hivyo vya afya walitoroka maeneo hayo kwa kuhofia usalama wao.

Tangu mwaka huo, jamii ya msitu wa Boni, hasa wanafunzi wamekuwa wakihangaika ni vipi wataipata elimu hadi kufikia upeo.

Ni mwaka huo wa 2014 ambapo Bi Nyokabi alifunganya virago kutoka kijiji chao cha Naro Moru, Kaunti ya Nyeri kuja Lamu, ambapo aliafikia kufungua biashara ya duka kijijini Mangai, ndani ya msitu wa Boni.

Kwa wakati huo, Bi Nyokabi alikuwa amehitimu masomo ya shule ya sekondari pekee (KCSE) ila hangeweza kuendeleza elimu yake kutokana na umaskini.

Baada ya wiki chache za kuishi kijiji cha Mangai, Bi Nyokabi aliguswa na jinsi watoto wa jamii ya Waboni walivyokuwa na kiu ya elimu ila changamoto tele zilikuwa zikiua ndoto na matumaini yao.

Hapa, mara nyingi shule zilisalia kufungwa ilhali zile chache zilizofunguliwa zikikabiliwa na changamoto tele ya uhaba wa walimu, madarasa na miundomsingi mingine.

Ni kutokana na hali hiyo ambapo Bi Nyokabi aliguswa kujitolea mhanga kusaidia wanafunzi Waboni wapate elimu bure bilashi.

Baada ya siku nzima ya kuuza dukani kwake, Bi Nyokabi alikuwa akikusanya wanafunzi Waboni kwenye nyumba mojawapo nyakati za jioni au usiku, ambapo alikuwa akiwapokeza mafunzo ya kuwasaidia darasani.

Haikuchukua muda mrefu, juhudi zake zilitambuliwa na jamii nzima na hata wakuu wa elimu na maafisa wa utawala eneo hilo.

Hapo ndipo jamii, maafisa wa elimu na wakuu wa utawala walipomrai kufika shuleni Mangai na kuanza kuwafundisha wanafunzi katika hatua ya kuwasaidia.

Bi Nyokabi aliitekeleza kazi hiyo ya kujitolea kwa miaka mitano, ambapo wakuu wa utawala na ofisi ya Mbunge wa Lamu Mashariki, Bi Ruweida Obbo, ilimtambua, hivyo kufadhili masomo yake ya taaluma ya ualimu.

Alijiunga na Chuo cha Walimu cha Islamic Teachers Training College kilichoko eneo la Mikindani, Kaunti ya Mombasa mnamo 2018.

Alifuzu taaluma ya ualimu na kupata cheti cha P1 mnamo 2020.

Baadaye alirudi kijijini Mangai, ambapo aliendelea kujitolea kufundisha shuleni humo hadi Januari 2023, ambapo aliajiriwa rasmi na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC).

Elizabeth Nyokabi Njogu, 38, ni mja aliyejitolea kwa hali na mali ilmuradi aifikishe elimu kwa jamii. Picha| Kalume Kazungu

Kwa sasa Bi Nyokabi ndiye mwalimu wa pekee wa kike kati ya walimu 26 wanaohudumia shule tano za msitu wa Boni.

Shule hizo ni Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, na Kiangwe.

Lakini je, kwa nini Bi Nyokabi kavalia moyo wa ushujaa na kuhudumia eneo ambapo hata walimu wanaume wanaogopa kufunza kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na Al-Shabaab?

Anataja huruma na ari ya kutaka kuibadilisha jamii ya Waboni kutoka kwa maisha ya ukale hadi kuibukia usasa kupitia elimu kuwa msukumo mkuu unaomfanya kuendelea kuhudumu msituni Boni miaka yote.

Anaeleza kuwa kila ajipatapo darasani akifunza na anapotazama kuona nyuso za watoto Waboni zilizosheheni furaha, hilo pekee humfanya kusahau kwamba yuko eneo lenye utovu wa usalama.

“Mimi hukumbuka tu kwamba niko pabaya wakati ninapotoka darasani. Nia yangu ni kuhakikisha elimu inawafikia vilivyo Waboni nikiamini fika kuwa ni kupitia hiyo elimu ambapo jamii hii itabadilika pakubwa na kufikia maendeleo kama jamii zingine nchini,” akasema Bi Nyokabi.

Ikumbukwe kuwa jamii ya Waboni inatambulika kwa kuendeleza maisha ya jadi na yanayoonekana kuwa ya kishamba, ambapo kitega uchumi cha jamii hii kimekuwa ni kuwinda wanyamapori, kuchuma matunda ya msituni na kuvuna asali ya mwitu.

Anawasihi walimu wenzake wa jinsia ya kike kuondoa shaka na badala yake kupiga moyo konde na kujitolea kufika msitu wa Boni kuwapokeza watoto elimu.

“Mbali na kujitolea kwangu kufundisha, uwepo wangu kama mwalimu wa kike hapa msitu wa Boni ni jambo muhimu. Hilo limewatia moyo wanafunzi wa jinsia ya kike kutia bidii zaidi masomoni wakijua fika kuwa pia wanaweza,” akasema Bi Nyokabi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mangai, Bw Khamis Mwaleso alimsifu Bi Nyokabi kwa ushujaa na bidii kazini.

“Amekuwa kielelezo kwa elimu ya mtoto wa kike. Ni kioo cha jamii eneo hili. Tunampenda Bi Nyokabi,” akasema Bw Mwaleso.

Naye Mkurugenzi wa Elimu, Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri alimtaja Bi Nyokabi na walimu wengine wanaohudumia shule za msitu wa Boni kuwa wazalendo, mashujaa na watu ambao kujitolea kwao kunafaa kupewa utambulishi maalum.

“Nawashukuru hao walimu kwa uzalendo na kujitolea kwao kuhakikisha jamii ya Boni inapata elimu. Ofisi yangu itafanya kila jitihada kuona kwamba maslahi ya walimu hao yanazingatiwa, kulindwa na kutimizwa kikamilifu,” akasema Bw Mutuiri.

Shule zote za msitu wa Boni zina zaidi ya wanafunzi 400 kutoka chekechea hadi Gredi 6.

Bi Nyokabi ni mama wa watoto watatu.

Ni mzawa wa tisa katika familia ya watoto 11.

Alisomea Shule ya Msingi ya Gitinga iliyoko Naro Moru, Nyeri na kisha kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kerugoya alikohitimisha masomo yake ya upili.