Habari za Kaunti

Familia 700 zapata nyaraka za umiliki wa ardhi baada ya miaka 40 Nanyuki

Na MWANGI MUIRURI September 8th, 2024 1 min read

ZAIDI ya familia 700 kutoka mtaa wa mabanda wa Likii, mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia wamepewa barua za kuonyesha wanamiliki vipande vyao vya ardhi huku mchakato wa kuhakikisha wanapata vyeti vya umiliki ardhi ukianza rasmi.  

Gavana wa Laikipia Joshua Irungu aliwaongoza maafisa wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi Nchini (NLC) kuwapa wakazi hao barua hizo huku wakisubiri vyeti vyao vya umiliki.

Kwa kipindi cha miaka 40 wanasiasa wamekuwa wakitumia suala la kuwapa wakazi hao hatimiliki kama chambo cha kuvutia kura zao.

“Leo ni siku nzuri kwa wakazi wa Likii kwa sababu ndoto yao ya miaka 40 imetimia. Mkiwa na vyeti vya kumiliki ardhi ambavyo vipo njiani, unaweza kuomba hata mkopo kwa benki,” akasema Gavana Irungu, ambaye amekuwa akilalamikia Rais William Ruto kuhusu kucheleweshwa kutolewa kwa vyeti hivyo.

Gavana alisema zaidi ya familia 1,000 nyingine ambazo zinaishi mtaa huo pia zingepokea barua hiyo lakini waliwasilisha kesi kortini kuhusiana na mzozo wa vipande vya ardhi.

Bw Irungu aliwaomba waondoe kesi hizo ili kuwe na maelewano ili nao wapokee barua wakisubiri vyeti vya umiliki.

Bi Wanjiru Ndegwa ambaye alikuwa kati ya waliopokea barua alikuwa na furaha akisema amesubiri kwa zaidi ya miaka 30.

Mtaa huo ulianza kuchipuka mapema miaka ya 60 wakati ambapo watu walikuwa wakihamia mjini Nanyuki.

Walijitwalia ardhi bila vyeti vya umiliki na wakakataa kuondoka.

Kwa miaka hiyo yote wamekuwa wakiishi wakiwa na hofu ya kufurushwa na serikali.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo