Habari Mseto

Familia ya afisa wa Wizara ya Hazina ya Kitaifa aliyeuawa yaomba haki

Na RICHARD MUNGUTI September 4th, 2024 1 min read

FAMILIA ya mfanyakazi wa Wizara ya Hazina ya Kitaifa Evans Chirchir aliyeuawa katika mazingira tata inaomba polisi wachunguze kisa hicho kwa kina ili haki itendeke.

Kupitia kwa mawakili Felix Keaton na Philip Langat, iliambia wanahabari katika mahakama kuu ya Milimani kwamba “Chirchir alikuwa amemweleza ndugu yake anahofia maisha yake kutokana na zabuni ya Sh286milioni aliyokuwa anashughulikia.”

Keaton alisema Chirchir alitoweka wikiendi na maiti yake ilikutwa katika mochari Machakos.

“Marehemu aliitwa na marafiki asafiri hadi Machakos. Mara ya mwisho alionekana akiwa hai mnamo Agosti 31, 2024,” Keaton aliambia wanahabari Jumanne, Septemba 3, 2024.

Wakili huyo alifichua kwamba familia ya marehemu ilikuwa imefikiria alikuwa ametiwa nguvuni na polisi baada ya kutorejea nyumbani Ijumaa, Jumamosi, Jumapili na Jumatatu (Septemba 2, 2024).

“Familia ilikuwa imetusihi tuwasilishe ombi katika mahakama kuu kuomba polisi wamfikishe kortini mwendazake iwapo wamemzuilia,” alisema Keaton.

Wakili huyo alisema walikuwa wameshtaki serikali lakini imebidi waondoe kesi hiyo.

“Tunaomba Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) achunguze kwa haraka mauaji ya Evans,” Keaton alimrai Mkurugenzi wa DCI kwa niaba ya familia.