Habari za Kitaifa

Fumbo: Mshukiwa mkuu wa mauaji Kware hajapatikana siku 30 baadaye

Na KAMORE MAINA September 22nd, 2024 2 min read

SIKU 30 tangu mshukiwa mkuu katika mauaji ya Kware, Nairobi, Collins Jumaisi Khalusha kutoroka kutoka kizuizini Gigiri katika mazingira ya kutatanisha, bado hajapatikana.

Imebainika kuwa Maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliopewa jukumu la kumsaka Jumaisi, 33 wamerejea katika vituo vyao vya kazi Nairobi.

Hili limezua maswali kuhusu jinsi mshukiwa kama huyo anaweza kuruhusiwa kuzurura huru kwa wiki kadhaa.

Maafisa kutoka Ofisi ya Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi (CRIB) na Kitengo cha OSU kwa sasa nao wanaonekana kulegeza kamba.

Juhudi za kumsaka Jumaisi ziliendelezwa hadi Kaunti ya Busia ambapo dokezi za awali zilionyesha kuwa alikuwa, lakini hakupatikana huko.

Nyumbani kwao kijijini, Kaunti ya Vihiga, wapelelezi waliwahoji jamaa za mshukiwa huyo ila waliohojiwa wakasema kuwa hawajamwona tangu alipotoroka katika seli za polisi za Gigiri mnamo Agosti 20, 2024, pamoja na raia wengine 12 kutoka Eritrea.

Ndugu zake waliambia wapelelezi kwamba Jumaisi hajawasiliana nao tangu atoroke, kuhepa kwake kukisababisha maafisa kadhaa kuhamishwa.

Mpelelezi mmoja aliambia Taifa Jumapili kwamba jamaa za Jumaisi wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kuhangaishwa na wanakijiji, ambao wakati fulani walitishia kuwashambulia ikiwa wangemruhusu mwanamume huyo nyumbani kwao.

“Sisi (wachunguzi) bado hatujapata habari kuhusu mahali ambapo mtu huyo anaweza kujificha. Hatumii simu na hata wananchi hawatoi taarifa zozote,” alisema mpelelezi huyo.

Mkuu wa DCI, Mohammed Amin, ametangaza zawadi ya pesa taslimu kwa yeyote atakayetoa taarifa za kuaminika kuhusu mahali alipo Jumaisi.

Wiki mbili zilizopita, wapelelezi kutoka OSU walikaa katika mpaka wa Kenya na Uganda Malaba kwa muda wa wiki moja baada ya taarifa kutoka kwa DCI kuashiria kuwa Jumaisi alionekana akijaribu kuvuka mpaka kuingia Uganda. Hata hivyo, hakuonekana.

Afisa mwingine pia aliarifu Taifa Jumapili kwamba mchakato wa kumsaka Jumaisi umefikia kikomo, ishara kwamba Wakenya wanaweza kuridhika na fumbo la mauaji ya Kware.

Hii ni baada ya wachunguzi kukosa kupata habari zozote muhimu na za kuaminika kuhusu mwanamume huyo.

Katika Kaunti ya Nairobi, uchunguzi kuhusu kutoroka kwa Jumaisi na wafungwa wengine 12 mnamo Agosti 20, 2024 pia umegonga mwamba.

Hii ni kwa sababu bado hawajapata ushahidi wowote unaomhusisha mshukiwa wa mauaji hayo na afisa yeyote kati ya wanane wa polisi wa kituo cha Gigiri waliokuwa kazini usiku huo.

DCI imefanya uchanganuzi kuhusu simu za mkononi za maafisa wanane wa polisi waliokuwa kazini siku hiyo.

Miongoni mwa wanane hao ni; maafisa watatu wakuu wa polisi ambao ni pamoja na mkuu wa kituo (OCS), kamanda wa polisi wa Gigiri (OCPD) na afisa wa zamu katika kituo cha polisi.

Maafisa hao watano Gerald Mutuku, Zachary Nyabuto, Mollent Achieng, Evans Kipkirui na Ronald Babo wamefikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200, 000 kila mmoja huku uchunguzi ukiendelea.