Habari za Kitaifa

Gachagua afanya mahesabu ya kumchumbia Raila kisiasa 2027

Na MWANGI MUIRURI August 6th, 2024 3 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anasema kuwa yuko tayari kumkumbatia kisiasa Kinara wa Upinzani Raila Odinga na atamfikia ili washirikiane naye katika uchaguzi wa 2027.

Kauli hiyo ya Bw Gachagua inakuja wakati ambapo Bw Odinga ameanza kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto na hata wandani wake wakateuliwa serikalini.

Naibu Rais alisema kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani si adui wa Mlima Kenya jinsi ambavyo imekuwa ikifasiriwa huku akidai alipotoshwa ndiposa amekuwa akimpinga katika siasa za nchi.

“Mimi nimekuwa nikibeba ile dhana kwamba Bw Odinga sio mtu wa kuaminiwa au wa kushirikiana naye kisiasa. Ndiyo sababu sisi katika eneo la Mlima tumekuwa tukijitenga naye,” akasema Bw Gachagua.

Alikuwa akizungumza mnamo Jumapili usiku, Agosti 4, 2024 wakati alipokuwa akihojiwa na runinga ya Inooro ambayo inapeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

“Kwa sasa nataka ieleweke kwamba Bw Odinga ni mmoja wa marafiki wetu ambao hata tunaweza kushirikiana naye kisiasa siku zijazo. Tumemkumbatia kama jamii kwa sababu Rais Ruto amemleta ndani ya serikali na tutachapa kazi pamoja na hatimaye muda ukifika, tuongee kuhusu ndoa kwa siku zijazo za miereka ya kisiasa,” akaongeza.

Bw Gachagua amekuwa hasimu mkubwa wa kisiasa wa waziri huyo mkuu wa zamani na alikuwa kati ya wanasiasa waliomtahadharisha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya kufanya kazi na kiongozi huyo wa ODM.

Kile ambacho kimeunganisha Naibu Rais na Bw Odinga kimtazamo ni wote kuunga mkono ugavi wa mapato kwa kutegemea idadi ya watu wala si ukubwa wa eneo.

Wito huo umemweka Bw Gachagua pabaya na baadhi ya wanasiasa katika kambi ya Kenya Kwanza, wengi wakimwona kama anayepigania tu maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya.

“Tumefunguka macho sasa na nitaongoza harakati za kumpendekeza Bw Odinga kama mshirika wetu wa dhati Mlimani kama ilivyokuwa katika kinyang’anyiro cha 2022 akisaidiana na Bw Kenyatta,” akasema.

Wakati wa mahojiano hayo, Naibu Rais alirejelea kauli yake kuwa alikuwa amemwekea Bw Odinga mtego kwenye ikulu.

Alisema ni Rais Ruto ndiye alimshauri ayatoe matamshi hayo na kwa kweli aliwajibika kwa kuwa kiongozi wa nchi na Bw Odinga walikutana Uganda kwa Rais Yoweri Museveni.

Alifunguka na kusema kuwa hatua ya Bw Odinga kuunga kauli yake kuhusu mgao wa rasilimali ni ishara tosha kuwa waziri huyo mkuu wa zamani anafahamu masuala ya uongozi wa nchi hii.

“”Nilikemewa sana hata na viongozi wenzangu wa Mlima Kenya. Lakini nilishangaa kumsikia Bw Odinga akiniunga mkono hadharani,

“Bibi yangu aliniambia kwamba roho imemfunulia kwamba Bw Odinga ni yule malaika wa nia njema ambaye kumtambua ni lazima kuwe na ufunuo. Ufunuo huo ndio hatujawahi kuwa nao kama watu wa Mlima na ndipo tukamchukia,” akasema.

Sifa hizi kochokocho ambazo Bw Gachagua amemiminia Raila zinakuja wakati ambapo kumekuwa na madai kuwa naibu rais anapanga kuanzisha ndoa ya kisiasa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Licha ya kukita sana siasa zake eneo la Mlima Kenya, wakati wa mahojiano hayo, Bw Gachagua alifunguka na kusema yupo tayari pia kuanzisha ushirikiano na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Kiongozi wa DAP Kenya Eugene Wamalwa.

Kumkumbatia Bw Odinga kuna kuja wakati ambapo washirika wa mbunge huyo wa zamani wa Lang’ata nao wameteuliwa ndani ya serikali kutokana na ukuruba wake na Rais Ruto.

Kando na kutunukiwa mawaziri watano, mwanasheria mkuu mteule Dorcas Oduor pia anatoka Nyanza, ngome ya kisiasa ya Raila.

Pia kuna mabadiliko yanayotarajiwa ya makatibu wanaodumu serikalini ambapo inadaiwa kinara huyo wa upinzani atavuna vinono.

Bw Gachagua mwenyewe amekuwa akilalamika kuwa wandani wake wanahangaishwa na makachero wa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) pamoja na maafisa kutoka Shirika la Kijasusi (NIS).

Kati ya wandani wake aliosema wamekuwa wakifuatiliwa, kuhangaishwa na mawasiliano yao kurekodiwa ni Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na mwenzake wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru maarufu kama Meja Donk.

Wakati wa mahojiano hayo, Naibu Rais alionekana kuwa na tofauti kubwa na bosi wake akisema kuwa hata hakuhusishwa au kushauriwa wakati ambapo katibu mkuu wa chama cha UDA, Bw Cleophas Malala aling’atuliwa mamlakani wiki jana.