Habari za Kitaifa

Gachagua aitaka ODM kuunga sera za serikali ya Kenya Kwanza

Na CHARLES WASONGA September 6th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anawataka wafuasi wa chama cha ODM kuunga mkono kwa dhati, mipango na miradi ya serikali ya Kenya Kwanza kwa sababu baadhi ya wanachama wao wameteuliwa mawaziri.

Hii ni licha ya kwamba maafisa wa chama hicho, wakiongozwa na kiongozi wake, Raila Odinga, wamekuwa wakishikilia kuwa kingali katika upinzani, kwa misingi kuwa hakijatia mkataba wowote na serikali.

Akiongea mjini Mombasa, Alhamisi, Septemba 5, 2024 alipofungua Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo mwaka huu, Bw Gachagua alisema wabunge wa chama hicho pia wanafaa kuunga mkono sera za serikali.

“Rais William Ruto aliunda serikali inayoshirikisha kila mtu. Hapa Pwani mkapewa mawaziri Salim Mvurya na Hassan Joho. Sasa wengi wenu ambao ni wanachama wa ODM mko ndani ya serikali na mnawafaa kuunga mipango ninayoelezea hapa na yanayohusiana na sekta ya kilimo. Hiyo ndiyo maana ya kuwa ndani ya serikali,” akasema.

Baada ya kukabwa koo na maandamano ya vijana wa Gen Z waliokuwa wakipigania utawala bora, Rais Ruto aliwafuta kazi mawaziri na kuteua wapya waliojumuisha viongozi wanne wa ODM.

Wanasiasa hao ni; waliokuwa manaibu wa kiongozi wa chama hicho, Bw Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti John Mbadi, aliyekuwa kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi na aliyekuwa mwanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uchaguzi katika ODM Beatrice Askul Moe.

Bw Joho ni Waziri wa Uchumi wa Majini na Uchimbaji Madini, huku Bw Oparanya akiongoza Wizara ya Ustawi wa Vyama vya Ushirika.

Naye Bw Mbadi ni Waziri wa Fedha, huku Wandayi akihudumu kama Waziri wa Kawi na Bi Askul akisimamia Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

Kauli ya Bw Gachagua pia inakosa mashiko kisheria kwa sababu chama cha ODM hakijajiondoa rasmi kutoka kwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Isitoshe, katika Bunge la Kitaifa na Seneti wanachama wa ODM ndio wanashikilia uongozi wa mrengo wa wachache na kamati za kuhakiki utendakazi wa serikali.

Juzi, msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alifafanua barua aliyopokea afisini mwake ni ile ya kujiuzulu kwa watano hao kutoka nyadhifa zao katika ODM.

“Kulingana na rekodi zilizoko katika afisi yangu, ODM ingali miongoni mwa vyama 26 tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya,” Bi Nderitu akanukuliwa akisema.

Hata hivyo, katika ziara zake katika maeneo ya Pwani, Magharibi mwa Kenya na Nyanza, ambayo ni ngome za ODM, Rais Ruto alidokeza kuhusu uwezekano wa chama hicho kushirikiana na Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.