Habari za Kitaifa

Gachagua: Wanaonitesa watanitafuta 2027 lakini nitazima simu

Na MERCY KOSKEI August 19th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewaonya wanasiasa wa Mlima Kenya ambao hakuwataja majina, ambao anasema wamekuwa wakipanga njama dhidi yake.

Kwa sababu hiyo, Naibu Rais amesema hatawaunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Gachagua alisema wanaomtesa watamtafuta 2027, na ikifika wakati huo, atazima simu yake wasimfikie.

Alifichua kuwa watu wengi aliowasaidia wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita ili kuchaguliwa, wamempa kisogo na wanapanga njama za kumporomosha.

“Kuna watu wengi niliowasaidia wakati wa kampeni wakashinda viti wanavyoshikilia leo. Lakini niligundua kuwa ni watu wale wale wanaopanga kuniangusha na kunishambulia,” akasema Bw Gachagua.

“Lakini jambo zuri ni kwamba uchaguzi unadumu kwa miaka mitano tu. Kwa hiyo watu hao watahitaji msaada wangu 2027. Nitawaunga mkono wale wanaoniunga mkono kwa sasa. Kuna watu wanasaidiwa na wanasaliti wengine. Mmoja wao hivi majuzi alikuwa na ujasiri wa kuuliza kwa nini sitambui kazi yake kila ninapotembelea eneo bunge lake,” aliongeza.

Bw Gachagua ambaye alizungumza sana kuhusu usaliti na udanganyifu katika siasa, hasa ndani ya muungano unaotawala wa Kenya Kwanza alisema : “Mimi binafsi nimeshuhudia siasa za usaliti na ujanja. Watu ambao nilisaidia kuchaguliwa ni baadhi ya watu ambao wamenisaliti. Lakini siasa ni hivyo, lazima uwe na uvumilivu.”

Akizungumza Jumamosi, wakati wa kumbukumbu ya marehemu David Chepkwony, mume wa Mbunge wa Njoro Charity Kathambi, Gachagua, alisema kuwa katika siasa, watu huwa na tabia ya kusahau kirahisi baada ya kupanda ngazi licha ya kusaidiwa na watu kufikia kiwango cha kuwatusi.

Alisikitika kuwa wanasiasa ni wepesi kuwasahau waliowasaidia kupanda ngazi lakini badala ya kuwaheshimu wanaanza kuwatukana, wakisahau uchaguzi ni baada ya miaka mitano.

Bw Gachagua hata hivyo alisema kuwa ataendelea kuwa rafiki na kufanya kazi na wale walio na ari ya kufanikisha na kusaidia mwananchi wa kawaida waliomchagua mamlakani.

Ufichuzi huo unajiri huku muungano unaotawala ukikumbwa na mzozo wa ndani, kukiwa na hali ya kutoelewana kati ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua amekuwa akiwasuta baadhi ya viongozi ambao anawashutumu kwa kuhujumu juhudi zake za kuunganisha eneo la Mlima Kenya.

Haya pia yanajiri huku kukiwa na madai ya kumuondoa madarakani Bw Gachagua, mchakato unaosemekana kuongozwa na wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya.

Wiki iliyopita, aliyekuwa Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleopas Malala alishutumu maafisa wakuu wa chama kwa kupanga kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Malala alilaumu Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa na Gavana wa Embu Cecily Mbarire kwa masaibu yake.

Huku akitaja kutimuliwa kwake ‘kinyume cha sheria’, mwanasiasa huyo mwenye msimamo mkali alidai kuwa wawili hao pamoja na washirika wengine walipanga njama ya kumuondoa kwanza, kabla ya kushinikiza kutimuliwa kwa Gachagua.