Habari za Kaunti

Gen Z walioshtakiwa na Sudi waomba korti iwapunguzie dhamana

Na TITUS OMINDE September 13th, 2024 1 min read

VIJANA tisa ambao walikuwa miongoni mwa washukiwa 16 waliokamatwa wakati wa maandamano ya Juni 25 jijini Eldoret wangali wanateseka katika gereza la Eldoret kwa kukosa dhamana.

Hii ni baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuiba na kuharibu mali ya thamani ya zaidi ya Sh150 milioni katika Klabu ya Timba XO ya Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.

Vijana hao wamewasilisha ombi katika Mahakama Kuu kutaka wapunguziwe dhamana.

Miezi miwili iliyopita, mahakama ya Eldoret iliwaachilia kwa dhamana ya Sh300,000 kila mmoja au dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh200,000.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuweza kutimiza masharti hayo na kumlazimisha wakili wa Eldoret, Kaira Nabasenge kuwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Eldoret.

Washtakiwa hao ni pamoja na Alfred Aloo, Ferdinand Lubisa, Annex Bornway, Martin Kabugi, Gideon Kiplimo, Joshua Majimbo, Brian Kimeli, Daniel Luta na Brian Rotich.

Bw Nabasenge ambaye alifika kortini mnamo Agosti 26 kupitia ombi la dharura alimweleza Jaji J Otieno vijana walioathiriwa ambao wana umri wa kati ya miaka 20 na 27 hawana uwezo wa kumudu dhamana ikizingatiwa kuwa wanatoka katika familia maskini.

Jaji Otieno aliidhinisha ombi hilo kuwa la dharura na akaagiza kwamba litasikizwa Septemba 16.

Wanakabiliwa na shtaka la pili la uharibifu wa mali uliojumuisha ofisi, chumba cha kudhibiti CCTV, duka kuu la Kilabu, pombe, viti, meza, miwani na vifaa vya kielektroniki vya aina mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya Sh80 milioni.