Michezo

Gor na Bandari wafahamu wapinzani wao Klabu Bingwa Afrika

July 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 18 wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia watasafiri hadi nchini Burundi kwa mechi yao ya raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika nao washindi wa Kombe la Ngao Bandari wazuru Sudan kwa Kombe la Mashirikisho la Afrika mwezi ujao.

Droo ya mashindano ya daraja ya juu ambayo ni Klabu Bingwa na yale ya daraja ya pili Kombe la Mashirikisho, zimefanywa jijini Cairo nchini Misri mnamo Julai 21.

Gor ya kocha Hassan Oktay italimana na Aigle Noir CS ambayo ilishinda Ligi Kuu ya Burundi kwa mara yake ya kwanza kabisa msimu 2018-2019.

Mshindi kati ya Gor na Aigle atajikatia tiketi ya raundi ya pili kumenyana na timu itakayoshinda USM Alger (Algeria) na SONIDEP (Niger).

Itakumbukwa ni mwaka 2018 tu pale Gor ilikutana na USM Alger katika mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho na kuikaba 0-0 jijini Nairobi kabla ya kupoteza 2-1 ilipozuru Algeria.

Mabingwa wa Kombe la Ngao mwaka 2015 na 2018 Bandari watakabiliana na Al Ahly Shandy katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho.

Bandari inarejea katika ulingo wa Afrika baada ya kuonekana mwaka 2016 pia katika kombe hili la daraja ya pili. Ilichapwa 2-0 na FC Saint-Eloi Lupopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi ya kuingia raundi ya kwanza kabla ya kuaga mashindano hayo ilipokabwa 1-1 jijini Nairobi.

Mshindi kati ya Bandari na Shandy atalimana na mshindi kati ya US Ben Guerdane (Tunisia) na Amarat (Sudan Kusini) katika raundi ya kwanza.