Habari za Kitaifa

GSU motoni kwa kunyemelea msichana wa shule

March 6th, 2024 2 min read

NA JESSE CHENGE

POLISI wa kupambana na ghasia (GSU) ametiwa mbaroni kwa kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi wa umri wa miaka 17 eneo la Mt Elgon katika Kaunti ya Bungoma.

Raia walimfumania afisa huyo akiwa na mwanafunzi huyo katika chumba cha jengo mojawapo eneo hilo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Kopsiro Justus Njeru, alisema kuwa afisa huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kipsigon wakati uchunguzi ukiendelea.

“Nilipigiwa simu kutoka kituo cha polisi cha Kipsigon ambapo mkuu wa pale alinipa taarifa kwamba alikuwa amepokea simu kutoka kambi ya GSU ya Chepkurkur kwamba afisa mmoja alikuwa amenaswa na wananchi akiwa na msichana wa shule katika nyumba ambayo walishukiwa kuwa pamoja,” akasema Bw Njeru.

Baada ya kukamatwa kwa mshukiwa, ambaye jina lake halijafichuliwa, mwathiriwa alipelekwa katika Hospitali ya Kopsiro, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa matibabu na ripoti ikaandaliwa.

Bw Njeru aliongeza kuwa fomu ya P3, pamoja na taarifa za mwathiriwa na mama yake, ziko tayari.

“Hadi sasa tumepokea fomu ya P3 kutoka kwa afisa wa matibabu, taarifa ya msichana husika pamoja na taarifa ya mama yake,” aliongeza.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Bungoma Jenipher Mbatiany, alilaani tukio hilo na kuomba uchunguzi wa haraka.

Alipongeza maafisa wa usalama Mt Elgon kwa kuchukua hatua haraka kwenye kesi hiyo ya afisa kumnyemelea mwanafunzi, tena wa umri chini ya miaka 18.

Bi Mbatiany alisisitiza umuhimu wa haki katika kesi kama hizo na alionyesha wasiwasi wake juu ya ongezeko la matukio ya aina hiyo, akiyataja kuwa yanalemaza elimu na kuchangia mimba za utotoni na kuenea kwa maradhi.

“Tunataka haki kwa mtoto huyu mdogo. Hili ni jambo la kusikitisha sana kwamba tunapopambana na visa kama hivi katika jamii zetu, bado kuna wale wanaoendelea kufanya mambo hayo,” alisema Bi Mbatiany.

Kiongozi huyo alihimiza mamlaka kuchunguza kesi hii kwa kina, kuhakikisha kwamba ukweli unafichuliwa na mshukiwa anakabiliwa na adhabu kali iliyo halali kisheria.

Alieleza kuwa matokeo ya kesi hii ni ya maslahi makubwa kwa umma, na akasisitiza umuhimu wa kukabiliana na visa kama hivyo katika jamii.

“Kila mtu hapa anataka kuona jinsi kesi hii itakavyokamilika, mtuhumiwa lazima awe mfano kwa wengine,” akasema.

Uchunguzi dhidi ya GSU huyo kujihusisha kimapenzi na mtoto mdogo unaendelea.