Habari Mseto

DHAHABU FEKI: Washukiwa ndani hadi Juni 27

May 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Munguti

WASHUKIWA 16 wa kashfa ya dhahabu feki Jumanne walisukumwa gerezani hadi Juni 27 mahakama itakapoamua hatima yao ya dhamana.

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi, aliamuru afisa wa urekebishaji tabia awahoji washukiwa wote ibainike hali ya kila mmoja.

“Hii mahakama imefahamishwa miongoni mwa washtakiwa ni wanafunzi, wengine ni walinzi, wengine ni madereva wa teksi na wengine ni wafanyakazi wa nyumbani na hawawezi kupata dhamana ya juu,” alisema Bw Andayi.

Bw Andayi alisema, “ili mahakama iweze kutenda haki kwa washukiwa hao, ripoti ya kila mmoja wa afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe mahakamani Mei 27, 2019.”

Hakimu alisema ni vyema kila mmoja wa washukiwa hao atendewe haki kulingana na msimamo wake katika jamii.

Walioshtakiwa ni pamoja na mfanyabiashara Jared Kiasa Otieno kwa ulaghai wa Sh300 milioni.

Shtaka la kwanza lilisema 16 hao walifanya njama za kumlaghai mfanyabiashara Sounthorn Chanthavong Sh300 milioni wakitumia ujanja.

Shtaka lilisema kati ya Februari 8 na 25, 2019 jijini Nairobi, walimwonyesha Bw Chanthavong, mkurugenzi wa kampuni ya Simuong Group fito feki vya dhahabu na masanduku ya chuma wakidai yalikuwa yamepakiwa dhahabu wakijua ni uwongo.

Bw Otieno pamoja na Philip Aroko, Robert Ouko ajulikanaye pia kama Paul Ouko Owiti na Rickey Thomas Okoth almaarufu Tom Okot walikabiliwa na shtaka la kumlaghai Bw Chanthavonmgo wakidai watamuuzia dhababu halisi.

Washukiwa wengine wote 15 walishtakiwa kwa kupatikana na stempu feki za idara ya forodha ya nchi ya Ghana wakidai zilikuwa halisi.

Pia, walishtakiwa kupatikana na vyuma na fito feki za dhahabu katika jumba la Kaputei Gardens, mtaani Kileleshwa kaunti ya Nairobi wakiwa na bidhaa bandia walizotumia kuwalaghai watu.

Washukiwa hao walimwonyesha mfanyabiashara huyo dhahabu hiyo feki katika kampuni ijulikanayo kama Nirone Safe Keeping Limited.

Shtaka lilisema washtakiwa walidai walikuwa wanafanya biashara ya dhahabu.

Jumla ya washukiwa 16 walifikishwa mahakamani wakiwemo raia watatu kutoka mataifa ya Congo na Chad.