• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
2TS Sacco yapunguzia abiria nauli

2TS Sacco yapunguzia abiria nauli

Na LAWRENCE ONGARO

MAGARI ya uchukuzi ya 2TS Sacco yanayohudumu mjini Thika – Thika Town Service – yamepunguza nauli kwa wasafiri kwa kukata asilimia 30.

Katibu wa 2TS Sacco, Bw David Nduati, alisema janga hili la Covid-19 limewalazimisha kuwajali wateja wao wa kila siku ambao ni abiria.

Baadhi ya maeneo yaliyopata afueni hiyo ni matatu za kwenda Thika-Makongeni, Thika- Landless, Thika-Kiganjo, na Thika-Muthaiga.

Alisema kwa muda wa siku tatu sasa, wameamua kwa kauli moja kuchukua hatua hiyo kwa sababu wananchi wengi kwa wakati huu wanapitia wakati mgumu ajabu.

Alisema katika ruti hizo za usafiri, wamepunguza nauli kati ya Sh10 na Sh 20 ili kuwapa wasafiri nafasi ya kujikimu.

“Tunaelewa maeneo mengi ya biashara watu wamekosa kupata faida yoyote. Na kwa hivyo, sisi kama washika dau wa sekta ya usafiri, tumewajali wateja wetu pia,” alisema Bw Nduati.

Alisema ya kwamba katika kila kituo cha kuabiri matatu, wanazidi kuhimiza wasafiri kunawa mikono bila kushurutishwa.

“Tunaiomba serikali ya Kaunti ya Kiambu ifanye hima ili kuleta jeli ya kusafisha mikono kwa wingi ili wananchi waweze kunawa mikono bila shida,” alisema Bw Nduati.

Dkt Susan Gitau ambaye ni mhadhiri katika chuo cha Nazarene jijini Nairobi na pia ni mshauri wa kisaikolojia, aliwasahuri wanachi wasitie hofu akilini mwao, bali wafuate sheria zote zilizowekwa kuzuia uchafu.

Dkt Susan Gitau ambaye ni mshauri awahamasisha wananchi kuhusu Covid-19 mjini Thika Machi 19, 2020. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tujaribu kujizuia kutokuwa na hofu, lakini tufuate maagizo ya serikali ya kuzingatia usafi kila mara hasa kunawa mikono kila mara. Pia tuepuke uvumi ambao unatuongezea hofu zaidi,” alisema Dkt Gitau.

Alisema pia watu wasimsahau Mungu Mwenyezi wakati wowote kwa sababu yeye ndiye chanzo cha matumaini zaidi ya wao kuishi.

“Kila mmoja wetu aweke imani mbele ili tuwe na matumaini ya kuzidi kuishi. Tusitie hofu katika nafsi zetu,” alisema Dkt Gitau.

Uchunguzi uliofanywa katika duka nyingi za jumla ni kwamba wateja wengi wananunua vyakula kwa wingi na dawa ya sanitizer ya kunawisha mikono.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Bw Alfred Wanyoike, alsema ameridhishwa na jinsi wananchi wanavyofuata mwito wa kunawa mikono.

“Nimezunguka mji wa Thika na kupata ya kwamba kila sekta ya biashara inafuata mwito wa kusafisha mikono jinsi walivyohimizwa na serikali,” alisema Bw Wanyoike.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wote wasiongeze bei ya bidhaa zao na huduma wanazotoa huku akisema wananchi kwa wakati huu wanapitia wakati mgumu.

“Tayari nimezunguka kote na kupata ya kwamba wananchi wengi wanakwenda katika supamaketi na kununua vyakula kwa wingi na jeli ya kutumika wakati wa kunawa pamoja na sabuni ya kipande,” alisema Bw Wanyoike.

Alitoa mwito kwa washika dau wote wanaofanya biashara waendelee kuuza bidhaa zao kwa bei ya kawaida bila kupandisha bei.

  • Tags

You can share this post!

Modern Coast yazima safari za Uganda, Rwanda na Tanzania...

KIKOLEZO: Corona yapiga stopu showbiz

adminleo