Starehe Boys Centre yasherehekea miaka 60 tangu ianzishwe
Na GEOFFREY ANENE
SHULE ya Upili ya Starehe Boys Centre leo Jumamosi inasherehekea miaka 60 tangu ianzishwe na mwendazake Dkt Geoffrey Griffin, huku ikitoa mwito kwa Wakenya kuisaidia kuchangisha Sh10 milioni iweze kuendelea na shughuli zake za kutoa elimu ya bure kwa watoto werevu kutoka jamii za kipato cha chini.
Mmoja wa wanafunzi wa zamani wa shule hiyo inayopatikana katika eneobunge la Starehe katika kaunti ya Nairobi, Paul Olungai, ambaye alisomea shuleni humo kutoka mwaka 1966-1979 na pia anahusika katika shughuli za uchangishaji wa fedha hizo, amefichua kuwa yeye pamoja na viongozi wengine kutoka shule hiyo wametembea umbali wa hadi kilomita 350 kuchangisha fedha hizo.
Starehe Boys huchukua wanafunzi waliopata alama 400 kuenda juu kwenye mtihani wa kitaifa.
Olungai, ambaye alikuwa akizungumza nje ya Makavazi ya Kitaifa ya Kenya kwenye barabara ya Moi Avenue, alitaka wanafunzi waliopata alama hizo kufika katika shule hiyo ya wavulana na kujaza fomu ya rangi ya manjano ya kuomba kusomea katika shule hiyo kabla ya mwezi huu wa Julai kutamatika.
Shule ya Starehe Girls, ambayo pia inapatia watoto wasichana kutoka jamii za kipato cha chini elimu ya bure, itakuwa na mchakato wa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Agosti.
Kiambu
Starehe Girls, ambayo ilianzishwa mwaka 2005, inapatikana katika Kaunti ya Kiambu.
Kabla ya Olungai kuzungumza pamoja na kutambulisha viongozi wa wenzake kutoka Chama cha Ushirika cha Wanafunzi wa zamani wa Starehe Boys Centre, Old Starehian Society, wanafunzi wa sasa kutoka shule hiyo ya wavulana walitumbuiza watazamaji kwa nyimbo mbalimbali kupitia ala za muziki zikiwemo tarumbeta, ngoma na saksafoni.
Thomas Mboya, ambaye aliuawa mwaka 1969, alikuwa mlezi wa kwanza wa Starehe Boys Centre. Tangu wakati huo, Rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki ndiye amekuwa mlezi wa shule hii.