Habari MsetoSiasa

Mbunge kujenga vyoo vipya kuokoa shule

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SHABAN MAKOKHA

MBUNGE wa Mumias Magharibi, Bw Johnson Naicca ameahidi kujenga vyoo vipya katika shule ya msingi ambayo serikali ilitaka kufunga kwa misingi ya kiafya.

Kuna hofu huenda wanafunzi zaidi ya 700 wa Shule ya Msingi ya Ingusi watakosa elimu shule zitakapofunguliwa kwani idara ya afya ya umma iliagiza shule hiyo ifungwe kwa kukosa vyoo safi.

Serikali iliahidi shule hiyo isifunguliwe hadi wakati vyoo vipya 12 vitakapojengwa.

Bw Naicca alisema ingawa kwa sasa hakuna pesa za kutosha, ameagiza kamati ya Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF) itafute pesa kokote ili ujenzi huo ufanywe kwa dharura.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw Richard Akwata alisema maafisa wa afya waliagiza vyoo sita vya wasichana na sita vya wavulana vijengwe ndipo shule ifunguliwe.

Shule hiyo kwa sasa ina vyoo 12 vya shimo ambavyo vimejaa kwani vinatumiwa pia na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Ingusi iliyo na wanafunzi karibu 500.