'Magavana hawajaridhia kaunti kupewa Sh316 bilioni'
Na STANLEY KIMUGE
MWENYEKITI wa Baraza la Magavana (CoG), Wycliffe Oparanya, amesema magavana hawakuridhishwa na hatua ya seneti ya kukubali pesa walizotengewa na bunge na kwamba ni mageuzi ya katiba tu yatakayohakikisha serikali za kaunti zimetengewa pesa za kutosha.
Bw Oparanya alisema kuwa magavana wanaunga mkono mchakato wa marekebisho ya katiba kwa jina Ugatuzi Initiative unaolenga kupiga jeki ugatuzi.
Kupitia mchakato huo, magavana wanataka kaunti ziwe zikitengewa asilimia 45 ya mapato ya serikali ya kitaifa kila mwaka.
“Tumekutana kujadili yaliyotokea katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na tukabaini kuwa serikali za kaunti hazijaweza kupata fedha kwa sababu ya udhaifu katika bunge la sasa.
“Kupitia mpango wa Ugatuzi Initiative tunataka kuwe na ufafanuzi kamili kuhusu namna ugavi wa mapato kati ya ngazi hizo mbili za serikali utakavyofanywa bila kuwa na utata,” akasema Bw Oparanya alipohutubu wakati wa maonyesho ya kilimo na biashara katika Chuo Kikuu cha Eldoret.
Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kakamega, alisema masuala kuhusu ugavi wa fedha hayajaangaziwa vizuri na Jopokazi la Maridhiano (BBI) na mswada wa Punguza Mizigo ambayo inajadiliwa na Wakenya.
Bw Oparanya alifichua, Septemba 18, magavana watatangaza tarehe ya kuzinduliwa kwa mchakato wao wa kugeuza katiba, wa Ugatuzi Initiative.
Muafaka
Alisema hawajaridhika na muafaka kati ya wabunge na maseneta kwamba serikali za kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni katika mwaka huu wa kifedha, na kupendekeza kuwa ziongezewe pesa zaidi kupitia bajeti ya ziada hapo Januari 2020.
Alisema haja yao kuu ni kuhakikisha mwishowe Wakenya wamepata mpango bora utakaojali maslahi yao.
Wiki jana, maseneta walikubaliana na pendekezo la wabunge kwamba kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni zilizopendekezwa katika Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) uliochapishwa upya na bunge la kitaifa.
Mnamo Julai 15, magavana walielekea katika Mahakama ya Juu wakitaka ushauri kuhusu namna mapato ya kitaifa yanapasa kugawanywa kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.
Hii ni baada ya Bunge la Kitaifa kupuuzilia mbali pendekezo la Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kwamba kaunti zipate mgao wa Sh335 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020.