Wafungwa wanawake katika gereza la Thika wapewa stakabadhi za kimsingi
Na LAWRENCE ONGARO
WAFUNGWA wanawake wapatao 100 katika gereza la Thika Women Prison walikuwa na jambo la kutabasamu baada ya kupata vyeti vya kuzaliwa vya wana wao wachanga kutoka kwa Huduma Centre.
Wakati huo pia maafisa hao wa Huduma Centre waliwakabidhi kadi za hospitali za NHIF pamoja na kusajiliwa ili kupata kitambulisho cha kitaifa.
Siku hiyo iliwafaa wafungwa hao kwa sababu pia waliweza kupewa vifaa muhimu kama vipodozi, sabuni, na hata vifaa vya Toilet rolls.
Bi Monica Muthoni, 41, ambaye anatumikia kifungo cha miaka mitano kwa kushambulia mtu, anafurahia kupata mtoto mchanga wiki moja iliyopita akisema hiyo ni baraka kwake.
Mama huyo ambaye ana watoto saba anawashauri wanawake wenzake walio nje wawe watu wakarimu na wajiepushe na fujo ambayo yaweza kusababisha maovu.
“Ninawashauri wanawake wawe watu wa kutegemewa katika jamii na wasikubali kutekwa na hasira kwani husababisha maovu,” alisema Bi Muthoni.
Alijutia yale yaliyosababisha yeye kujipata gerezani lakini tayari ameomba msamaha wa kupunguziwa miaka ambapo hivi karibuni anaamini siku zake kutumikia zitapunguzwa.
Meneja wa Huduma Centre Kaunti ya Kiambu Bi Sharon Nzau aliwatetea wafungwa kwa kusema ya kwamba hata wao wana haki ya kupata vyeti muhimu vya kurahisisha serikali.
Alisema idara hiyo ilifanya juhudi kusajili wafungwa kadha na vitambulisho vya kitaifa – IDs – ambavyo vitawafaa wakati wowote wakikamilisha vifungo vyao vya gerezani.
Wakati huo pia watoto wapatao sita walisajiliwa na vyeti vya kuzaliwa huku akina mama zao wakifurahia mno.
Naibu afisa mkuu wa Gereza hilo Bi Doreen Ombati, alisema kuwa gerezani humo kuna wafungwa wanawake wapatao 150 na watoto wachanga 10.
Alisema watoto wanapotimiza umri wa miaka minne huregeshwa kwao nyumbani ama kuhifadhiwa katika kituo cha watoto.
Aliwahimiza wanawake kule nje wawe raia wema na wajiepushe na mambo ambayo yanaweza kusababisha hasira.
“Ni vyema kama mwanamke kujituliza nyumbani na majukumu muhimu badala ya kujihusisha na vurugu za kila mara,” alisema Bi Ombati.