Habari Mseto

46 wanyakwa kwa kuuza mafuta bila leseni

August 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Washukiwa 46 walikamatwa wakati wa operesheni katika vituo vitatu vya kuuzia mafuta ambavyo havikuwa na leseni.

Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) Jumatatu ilitekeleza operesheni hiyo katika vituo vitatu vya kuuzia mafuta ambavyo viko eneo la Salgaa, Kaunti ya Nakuru.

Operesheni hiyo ilitekelezwa kwa kushirikisha maafisa uchunguzi wa kihalifu (DCI) na maafisa wa polisi wa jumla(GSU).

Walipata lita 1,000 za mafuta yaliyokuwa yamechanganywa yakiwa yamehifadhiwa kwa vibuyu na mapipa.

Washukiwa watashtakiwa kwa makosa tofauti.

Baadhi ya makosa hayo ni kujenga hifadhi ya mafuta bila leseni, kuuza mafuta bila idhini pamoja, kupatikana na mafuta yaliyochafuliwa kinyume cha sheria, na kupatikana na mafuta ya kuuza nje ya nchi kinyume na sheria.