Ashtakiwa kuwapunja walalamishi zaidi ya Sh50 milioni
Na JOSEPH WANGUI
MTAALAMU wa masuala ya ubadilishanaji fedha aliyekamatwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) akiabiri ndege baada ya walalamishi zaidi ya 60 kwamba ni tapeli, amezuiliwa kwa siku nne baada ya kufikishwa mbele ya mahakama ya hakimu, Milimani, Nairobi.
Emmanuel Mulinge Maundu pia akifahamika kama Emmanuel Wambua Maundu amezuiliwa baada ya kukanusha mashtaka 68 ya kupokea zaidi ya Sh51 milioni akizingizia kwamba angewapa riba ya hadi asilimia 30 ya thamani ya pesa za walalamishi.
Alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu Nancy Nanzushi, amekanusha kwamba aliwalaghai walalamishi baina ya Januari na Agosti 2019, katika View Park Towers, Nairobi akiwa na wengine ambao hawakuwa mahakamani.
Mahakama imeambiwa alitekeleza makosa hayo akiwa mkurugenzi wa Forex Training and Consultancy Limited.
Baadhi ya walalamishi ni Bi Ann Wambui Mngolia aliyekuwa amempa Sh3 milioni na Bw Pius Mwangi Waititu aliyempa Sh100,000.
Maundu ameomba dhamana lakini mahakama ikasema hawezi akaachiliwa hadi ithibitishe usalama wake ikizingatiwa “wengi wanamuandama kwa makosa anayodaiwa kuyatekeleza”.
Amesema amekuwa akizuiliwa kwa siku tisa na kwamba kuendelea kuwa katika hali hiyo kunahatarisha afya yake.
“Naahirisha kusikizwa kwa masharti ya dhamana hadi idara ya uangalizi ilete ripoti kuhusu usalama wa mshukiwa endapo ataachiliwa kwa dhamana,” amesema Bi Nanzushi.
Kesi itatajwa Machi 10, 2020.