Habari Mseto

Staa wa Benga za Kikuyu Jimmy Wayuni afariki

May 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA SIMON CIURI

Mwanamuziki mtajika wa nyimbo za Benga za jamii ya Agikuyu Jimmy Walter alifariki katika ajali ya barabarani.

Msanii huyo anayejulikana na wafuasi wake kama Jimmy Wayuni aliaga dunia Jumanne usiku wakati gari lake lilipogonga lori eneo la Kahawa Sukari karibu na mtaa wa Githurai alipokuwa akielekea Nairobi akitoka Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Wayuni, ambaye ni Naibu Kamishena mstaafu wa Mamlaka ya Ushuru nchini [KRA] alikuwa amemsafirisha mwanamziki mwenzake, Jackson Kibandi aliyeponea ajali hiyo na kulazwa hospitalini.

OCPD wa Ruiru Phineas Ringera aliambia Taifa Leo kwamba mwanamziki huyo alikuwa anajaribu kutoka barabara kuu la Thika Githurai, alipongonga lori Githurai.

“Tumengundua kwamba alikuwa anaelekea Nairobi kutoka Ruiru, alikuwa anajaribu kutoka katika barabara ya Thika alipogongana na lori,” alisema Bw Ringera.

“Alikuwa ameumia sana na akakimbizwa hospitalini St Joseph alipoaga dunia akiendelea kutibiwa.”

Bw Ringera alisema kwamba mwili wa Wayuni ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mabaki ya gari lake yamewekwa katika kikuo cha polisi cha Kahawa.

Mwanamziki huyo alitamba sana kwa vibao vyake vya “Airitu a Ruiru” na “Wayuni Utuire Uhenagia”.