Habari Mseto

Abiria walia nauli ya Sh40 ya treni jijini Nairobi inawaumiza

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WATUMIAJI wa treni inayohudumu kutoka jijini Nairobi hadi mjini Ruiru katika kaunti ya Kiambu wamelalamikia hatua ya Shirika la Usafiri wa Treni la Kenya Railways kurejesha nauli ya awali ya juu bila kuwapa notisi.

Waziri wa Uchukuzi, James Macharia alitangazia Kenya Railways mnamo Novemba 12, 2018 ipunguze nauli ya Sh40 kwa asilimia 10.

Kutoka Novemba 13, 2018, abiria walianza kufurahia kulipia umbali wa safari hiyo ya kilomita 32 nauli ya Sh30.

Hata hivyo, abiria walipatwa na mshangao walipoanza kuitishwa Sh40 mnamo Januari 3, 2019. Baadhi yao, ambao ndiyo wamerejea kutumia treni hilo baada ya likizo, bado wanalalamika. “Tangu mwezi Novemba tumekuwa tukilipa Sh30. Inakuwaje mnalipisha nauli ya Sh40 leo hata bila ya kuweka ilani?” abiria mmoja alisikika akiuliza.

Mhudumu mmoja wa kukata tiketi alimjibu kwamba tangazo la Waziri Macharia lilikuwa tu ofa ya muda tu na wala haikuwa nauli mpya ya muda mrefu. “Hiyo ilikuwa ofa tu na imeisha.”

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Kenya Railways ilisema Januari 2 kwamba, “Huduma za treni (Nairobi Commuter Rail) zitarejea Januari 3, 2019”, ingawa haikufafanua nauli kurejeshwa hadi Sh40 katika barabara hiyo.

Nauli ilipunguzwa wakazi wa Nairobi walipotatizika kusafiri kufuatia mgomo wa magari ya kusafirisha abiria almaarufu matatu baada ya serikali kutangazia wamiliki wa magari hayo watimize sheria za trafiki za maarufu kama “Sheria za Michuki”.

Sheria hizo zinalenga kudumisha usalama barabarani na kuzuia ajali. Wamiliki wanastahili kuweka vidhibitimwendo katika magari yao pamoja na mikanda ya abiria, miongoni mwa masharti mengine, kabla ya kuhudumu.

Magari yalikuwa machache sana barabarani baada ya Wizara ya Uchukuzi kutoa tangazo hilo kwa wamiliki na kushuhudia abiria wengi wakiamua kutumia treni ambalo lilikuwa likijaa sana kabla ya wizara kuongeza idadi ya safari za treni hilo.