• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Abiria washerehekea Pasaka ndani ya seli jijini

Abiria washerehekea Pasaka ndani ya seli jijini

NA TAIFA RIPOTA

WASAFIRI wengi waliadhimisha Pasaka 2024 ndani ya seli za polisi baada ya kukamatwa kwa makosa mbalimbali ya trafiki.

Walinaswa na kikosi cha maafisa wa polisi na wale wa mamlaka ya kitaifa ya usalama barabarani (NTSA) Jumapili, Machi 31, 2024 asubuhi wakiwa wamesongamana katika matatu kwenye operesheni iliyoendeshwa katika barabara kuu ya Thika, maarufu kama Thika Super Highway.

Baadhi ya magari hayo hayakuwa na vyeti hitajika kutoka kwa NTSA na yalinaswa na nambari zao za usajili zikang’olewa.

“Hii ni operesheni ya kawaida inayoendeshwa kote nchini. Tunataka kuhakikisha kuwa kila Mkenya ni salama barabarani,” Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika NTSA Anthony Nyongsa akasema alipofikiwa kwa njia ya simu.

Tangu wiki jana, maafisa wa mamlaka hiyo wamejitokeza kupiga jeki juhudi za polisi kuhakikisha kuwa sheria za trafiki zinafuatwa kote nchini.

Mnamo Jumamosi jioni, Machi 30, 2024 madereva kadhaa walevi walikamatwa na kupimwa ulevi.

Akiongea katika barabara ya Kiambu siku hiyo, mkuu wa kitengo cha mikakati ya usalama barabarani Dkt Duncan Kibogong alisema mienendo ya madereva kuendesha magari wakiwa walevi ni hatari kwa usalama barabarani.

“Tutafanya kila tuwezalo kukomesha mienendo hii ili kuhakikisha kuwa barabara zetu ni salama,” afisa huyo akaambia wanahabari.

Majuma mawili yaliyopita Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema kuwa baadhi ya mikakati inalenga kupunguza ajali za barabarani na kurejesha ushirikiano kati ya NTSA na Polisi katika masuala ya usalama barabarani.

 

  • Tags

You can share this post!

Urafiki wa Joho, Omar wazua joto kisiasa

Polisi waokoa watoto 10 waliozuiliwa kanisani kwa...

T L