• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Abiria wataka huduma za treni Nairobi ziendelee kama kawaida

Abiria wataka huduma za treni Nairobi ziendelee kama kawaida

NA GEOFFREY ANENE

ABIRIA wa magarimoshi yanayohudumu maeneo ya Ruiru, Syokimau, Embakasi na Kikuyu hadi jijini Nairobi wametaka Shirika la Reli Kenya (Kenya Railways) lijikakamue kurekebisha matatizo yanayolifanya kukatiza huduma kwa ghafla kila mara mvua inaponyesha.

Wamelilaumu vikali wakitaka liende na wakati kiteknolojia. Abiria hao walielezea masikitiko yao baada ya kufika katika vituo vya kupanda magarimoshi hayo mapema Jumanne na kuyakosa.

“Tafuteni mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga. Mnafaa kufahamu kuwa teknolojia ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa. Chukulieni usafiri wa treni kwa uzito kwa sababu njia hii ni salama kuliko kutumia matatu,” alichemka abiria mmoja.

“Mmetueleza kuwa sehemu fulani za barabara zimejaa maji na kuwa garimoshi haliwezi kupita. Hii inamaanisha kuwa mmeshindwa kabisa na kazi ya kumaliza shida hiyo?” abiria mwingine aliuliza kwa hasira.

“Mbona hamuwezi kurekebisha haya magarimoshi,” alisema mtumiaji mwingine wa treni hizo.

Huduma za garimoshi jijini Nairobi zilitatizwa Jumanne baada ya barabara kujaa maji kutokana na mvua kunyesha usiku kucha.

Treni inayohudumia wakazi wa maeneo ya Syokimau hadi katika kituo kikuu ya Kenya Railways katikati mwa jiji ilisitisha safari zake baada ya mvua hiyo kufanya sehemu ya mtaa wa Mukuru kutopitika.

Wakaaji wa mitaa ya Embakasi walilazimika kutumia usafiri mbadala kufika mjini baada ya treni inayohudumu njia hiyo kukwama kwa sababu ya injini kukumbwa na matatizo, huku ile inayotumiwa na abiria wa kuelekea Kikuyu kupitia mtaa wa Kibera ikipata hitilafu sawa na hayo.

Treni inayohudumu barabara ya Ruiru katika kaunti ya Kiambu hadi jijini Nairobi pia inasemekana haikuhudumia wateja wake, ingawa Kenya Railways ilitangaza tu kuwa magarimoshi ya Syokimau, Embakasi na Kikuyu ndio yaliathirika.

“Usafiri utakuwa sawa kwa watumiaji wa treni kutoka mjini hadi Kikuyu leo jioni (Jumanne). Garimoshi la kuenda Ruiru pia litakuweko, lakini abiria wa Embakasi na Syokimau watalazimika kutafuta njia mbadala kwa sababu bado mambo hayajakuwa shwari katika sehemu fulani za reli,” afisa mmoja kutoka shirika hilo alisema.

Magari hayo huhudumia maelfu ya watu kila siku. Hata hivyo, yana historia ndefu ya kutatizwa na mafuriko mvua nyingi inaponyesha, hasa kutokana na mitaro inayopitisha maji kuziba baada ya wakazi kunyakua ardhi na kujenga nyumba zao karibu na reli. Nayo injini ya treni ya Embakasi ni ndogo haiwezi kukokota zaidi ya mabehewa 10.

You can share this post!

Kampuni za ulinzi zalia wateja wamekataa kulipia huduma

Corona ilivyozima ndoto za vijana

adminleo