Habari Mseto

Ada za juu zaanza kuwang’ata wanaosaka stakabadhi muhimu

March 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DANIEL OGETTA Na CHARLES WASONGA

WATU wanaosaka stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho vya kitaifa, pasipoti, vyeti vya kuzaliwa na kifo, vyeti vya kazi miongoni mwa vingine, sasa watagharimika zaidi baada ya serikali kuongeza ada zitakazotozwa huduma hizo.

Serikali imeongeza ada kwa wanasaka stakabadhi hiyo zaidi ya maradufu au hadi zaidi ya mara kumi ya ada za zamani.

Ada na matozo mapya yataanza kutumika baada ya kukamilishwa kwa vikao vya kukusanya maoni kutoka kwa umma.

Vikao hivyo viliendeshwa kati ya Novemba 14, 2023, na Desemba 5, 2023, kulingana na taarifa ya serikali iliyotolewa Februari 29, 2024.

“Unaweza kukumbuka kuwa tarehe ya utekelezaji wa hizo ada ilikuwa Januari 1, 2024. Hata hivyo, umma utapewa nafasi ya kutoa maoni kuhusu ada hizi katika kuanza kutumika,” ikasema taarifa hiyo kutoka kwa mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji katika Wizara ya Masuala ya Ndani.

“Kwa hivyo, lengo la taarifa hii ni kuwajulisha kuwa kuanzia Machi 1, 2024, ada mpya na matozo mengine yataanza kuitishwa kwa wanaowasilisha maombi ya stakabadhi husika,” akaweka wazi.

Nakala za taarifa hiyo zilitumwa kwa wakuu wa vitengo vyote, washirikishi wa kanda, afisi ya kitaifa ya usajili na wasajili na washirikishi katika ngazi za Kaunti na Kaunti ndogo.

Mnamo Novemba 14, 2023, Waziri wa Masuala ya Ndani Kithure Kindiki kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali nambari 241 alichapisha nyongeza ya ada kwa huduma zote zinazotolewa na idara ya uhamiaji.

Kwa hivyo, kuanzia Machi 1, 2024, ada mpya ya kupata cheti cha kuzaliwa itakuwa Sh200 kutoka Sh50, sawa na ada ya cheti cha kifo.

Wale ambao watatuma maombi ya cheti cha kuzaliwa kuchelewa watalipa Sh500 badala ya ada ya sasa ya Sh50, sawa na ombi la ada ya kifo kuchelewa.

Ada ya kuifanya marekebisho stakabadhi hizo imeongezwa kutoka Sh870 hadi Sh1,000.

Usajiliwa wa watoto waliozaliwa na watu waliokufa katika mabalozi wa Kenya katika mataifa ya kigeni utagharimu dola 150 za Amerika (Sh21,750) kutoka dola 50 (Sh7,250).

Ada ya kupata kitambulisho kingine cha kitaifa baada ya kile cha zamani kuharibika sasa ni Sh1,000.

Zamani huduma hiyo ilikuwa ikigharimu Sh100 pekee.

Hata ada ya kubadilisha maelezo kwenye kitambulisho cha kitaifa imesalia Sh1,000 ilivyokuwa zamani.

Kuanzia Machi gharama ya kupata paspoti ya kurasa 34 imepandishwa hadi Sh7,500 kutoka ada ya zamani ya Sh4,500.

Aidha, ada ya pasipoti ya kurasa 50 imepanda hadi Sh9,500 kutoka Sh6,000 huku ada ya maombi ya pasipoti ya kurasa 66 ikipanda hadi Sh12,500 kutoka Sh7,500.

Wakati huo huo, ada ya maombi ya pasipoti ya kidiplomasia yenye kurasa 50 imeongezwa maradufu hadi Sh15,000 huku ada ya pasipoti ya kidiplomasia ya kurasa 34 ikisalia Sh6,000 kama zamani.

Ili mtu kupewa pasipoti nyingine baada ya ile ya zamani kupotea atalazimika kulipa Sh20,000 kutoka ada ya sasa ya Sh12,000.

Aidha, ada ya kupata pasipoti mpya baada ya ile ya zamani kuchakaa imeongezwa maradufu hadi Sh20,000 kutoka Sh10,000.

Wakati huo huo, watumishi wa umma watatozwa Sh1,000 kupata beji za kazi kutoka ada ya zamani ya Sh350.