Afisa katika kesi ya ulaghai wa shamba la mabilioni ‘augua’
NA RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA Naibu Mkuu wa Mkoa wa Nairobi, Davis Nathan Chelogoi amepelekwa kupokea matibabu Nairobi Hospital kutoka Gereza la Viwandani baada ya kuugua.
Bw Chelogoi alipelekwa hospitali na maafisa wa idara ya magereza baada ya kupewa dhamana ya Sh10 milioni katika kesi ya ulaghai wa shamba la Sh1.35 bilioni.
Hakimu Mwandamizi, Dolphina Alego aliamuru mshtakiwa apelekwe Nairobi Hospital baada ya kufahamishwa “hakupata matibabu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kufuatia mgomo wa madaktari ambao umeingia wiki ya tatu.”
Hakimu alifahamishwa na wakili Prof Tom Ojienda kwamba Chelogoi aliugua Ijumaa (Machi 22, 2024) alipokuwa katika gereza la Viwandani ambapo alipelekwa Alhamisi wiki iliyopita, baada ya kukana mashtaka manane ya ulaghai wa shamba la wafanyabiashara Ashok Rupshi Shah na Hitenkumar Raja.
Shamba hilo Hakimu Alego alielezwa kuwa ni la ukubwa wa hekta 7.390, na la thamani ya Sh1, 350, 000, 000.
Mahakama iliambiwa kuwa shamba hilo liko eneo la Lower Kabete.
Akiwasilisha ombi, Chelogoi apelekwe Nairobi Hospitali, Prof Ojienda alisema “Mshtakiwa alipelekwa KNH lakini hakupokea matibabu na wala hakulazwa kufuatia mgomo wa madaktari”.
Alisema daktari wake alimtembelea katika Gereza la Viwandani na kumpima na kupata hali yake ya kiafya imeendelea kudorora.
Kiongozi wa Mashtaka Sonnia Njoki na wakili Suleiman Bashir alieleza mahakama “Afya ya mtu hupewa kipau mbele na kamwe hapingi mshtakiwa kupelekwa Nairobi Hospital”.
Hakimu aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitali chini ya ulinzi wa askari jela watu wa familia yake wakiweka mikakati ya kumlipia dhamana hiyo ya Sh10 mlioni na wadhamini wawili wa kiasi sawa na hicho.
Endapo mshtakiwa atashindwa kupata dhamana, mahakama ilimpa dhamana badala ya Sh5 milioni pesa tasilimu.