Habari Mseto

Afisa wa matibabu apatikana na hatia ya kutumikia ‘mabwana’ wawili

Na RICHARD MUNGUTI November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AFISA wa matibabu Jumatano Novemba 20, 2024 alipatikana na hatia ya kufungua kliniki cha kibinafsi akiwa angali ameajiriwa kutumikia umma katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki iliyoko mtaani Umoja III, Nairobi.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi, alimpata na hatia Charles Chacha Senso kwa kufungua kliniki kwa jina Eagle Mission Medicare (EMM) mtaani Kayole, Nairobi alipokuwa ameajiriwa kama afisa wa matibabu (Clinical Officer), katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki.

Pia, Bw Ekhubi alimpata Senso na hatia ya kupeana dawa kinyume cha sheria mnamo Aprili 3, 2021.

Akipitisha uamuzi, Bw Ekhubi alisema Senso alikaidi Kifungu cha Sheria Nambari 20(1) kinachopinga Afisa wa Matibabu kufungua hospitali ya kibinafsi na kutoa huduma sawa na anazotoa akiwa ameajiriwa kuhudumia Serikali.

Vile vile, Senso alipatikana na hatia ya kupeana dawa za kutibu maradhi ya Covid-19 kinyume cha sheria.

Akasema Bw Ekhubi: “Baada ya kuchambua ushahidi uliowasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki nimefikia uamuzi kwamba mshtakiwa yuko na hatia.”

Hakimu aliombwa na Bi Kariuki achukulie hilo kuwa kosa la kwanza kufanywa na Senso.

Badala ya kumhukumu mara hiyo, Bw Ekhubi aliagiza idara ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti kuhusu tabia ya mshtakiwa hapo awali kabla ya kupitisha hukumu.

Wakili Evans Ondieki anayemwakilisha Senso hakupinga ombi hilo la kuwasilishwa kwa ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia.

Bw Ekhubi aliamuru kesi hiyo itajwe Desemba 4, 2024 ili idara ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti kuhusu Senso.

Afisa wa urekebishaji tabia atamhoji mshtakiwa, watu wa familia yake, afisa wa utawala kama vile Naibu wa Chifu au wazee wa nyumba 10, kiongozi wa kanisa anakohudhuria ibada za Jumapili ama Sabato au imamu wa msikiti kupata taarifa kuhusu tabia ya awali ya mshtakiwa kabla ya kushtakiwa ndipo mahakama iweze kutoa uamuzi.

Ikiwa mshtakiwa atapatikana alihusika na uhalifu hapo mbeleni basi atasukumwa jela lakini akipatikana hajashiriki uhalifu hapo awali basi atapewa kifungo cha nje.

Katika kifungo cha nje, Senso atakuwa anaenda kupiga ripoti kwa afisa huyo wa urekebishaji tabia ashauriwe jinsi ya kutojihusisha na uhalifu.

Pia anaweza kuadhibiwa kufanya kazi katika afisi ya chifu kwa muda wote alioamriwa na mahakama.

Bw Ekhubi alimruhusu Senso kuendelea kukaa nje kwa dhamana hadi Desemba 4, 2024 atakapopitisha hukumu.