Afisa wa polisi afyatua risasi kuhepa na deni la pombe
NA WYCLIFFE NYABERI
POLISI eneo la Transmara, Kaunti ya Narok wanachunguza kisa ambapo afisa wa kitengo cha RDU (Rapid Deployment Unit) alifyatua risasi moja hewani alipodaiwa deni la pombe aliyokuwa amebugia katika baa moja.
Afisa huyo aliyetambulika kwa jina la Dennis Imai na aliyewekwa katika kambi ya RDU kijiji cha Enkorika, anasemekana kujilimbikizia bili ya Sh 2, 220 kutokana na chupa kadhaa za bia aliyokuwa ameinywa katika baa ya kuuza mvinyo iliyoko Lolgorian.
Mnamo Jumapili, Aprili 7, 2024 afisa huyo alirudi katika baa hiyo na mhudumu aliyekuwa amemuuzia, alipatwa na uchungu wa kutolipwa pesa zake.
Ili kumshurutisha Bw Imai amlipe, Bi Jackline Jemeli alimnyatia afisa huyo na kumpokonya simu yake.
Baada ya mabishano ya muda mfupi, afisa huyo ambaye alikuwa amevaa kiraia aliondoka.
Alirejea baada ya dakika 30 akiwa amevalia sare kamili za polisi huku akiwa amejihami na bunduki.
Duru zinaarifu alikuwa ameandamana na mwendesha bodaboda ambaye kufikia sasa hajatambulika.
“Alidai simu yake kwa nguvu na mhudumu alipokataa kumpa, alifyatua risasi moja na kisha kutoroshwa na bodaboda huyo aliyekuwa amesimama mita chache,” ilisoma sehemu ya ripoti ya polisi ambayo Taifa Dijitali ilifanikiwa kuiona.
Maafisa wa polisi kutoka Lolgorian walitembelea eneo la tukio lakini hawakumpata afisa huyo aliyekimbilia kusikojulikana.
Juhudi za kutafuta ganda la risasi hiyo iliyotumika ziliambulia patupu.
Ilishukiwa kuwa huenda afisa huyo alilichukua.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Transmara Kusini Charles Opondo aliahidi kutoa habari zaidi atakapowasili katika eneo lake la kazi.
“Sasa hivi ninaelekea eneo langu la kazi. Nimekuwa kwenye likizo. Tafadhali niruhusu nitoe taarifa zaidi kuhusu tukio hilo mara nitakapofika huko. Nitawaambia ikiwa afisa huyo amekamatwa au la. Lakini niliskia tukio hilo lilifanyika,” Bw Opondo aliambia Taifa Dijitali kwenye mahojiano kwa njia ya simu.