• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Afisa wa wizara ashtakiwa kuiba tikiti za tamasha

Afisa wa wizara ashtakiwa kuiba tikiti za tamasha

Na JOSEPH WANGUI

AFISA wa Wizara ya Elimu aliyedaiwa kuiba mabunda matano ya tikiti za kuhudhuria mashindano ya kitaifa ya tamasha ya muziki alishtakiwa jana katika mahakama ya Nyeri.

Tikiti hizo za kuhudhuria tamasha hiyo ya 92 inayoendelea katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi ziligharimu Sh12,500.

Bw Winfred Ombanda Ochieng, ambaye ni afisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika wizara hiyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkuu Phillip Mutua.

Alisomewa mashtaka mawili, ya wizii na kupatikana akiwa na mali ya wizi.

Alikanusha mashtaka akaachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 huku kesi ikipangiwa kutajwa Agosti 23.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Pauline Mwaniki, ulisema Bw Ochieng alitenda kosa hilo mnamo Agosti 8, 2018 katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi.

Bw Ochieng alipatikana katika tamasha hiyo na maafisa wa usalama akiwa anauzia wanafunzi tikiti ili waingie katika ukumbi kutazama mashindano ya muziki.

Aliekwa kizuizini na maafisa hao wa usalama akapatikana na Sh600 zinazoaminika alizipata kutokana na ulaghai huo.

Baadaye alipelekwa hadi katika kituo kikuu cha polisi cha Nyeri baada ya kufanyiwa mahojiano na waandalizi wa tamasha ambao walibainisha alipata tikiti hizo kupitia kwa ulaghai.

Mahakama iliambiwa aliweza kupata tikiti hizo kutokana na kuwa ni mfanyakazi katika wizara.

Mbali na hayo, mahakama pia iliambiwa afisa huyo alichukua mabunda hayo ya tikiti akifahamu wazi kwamba ni mali ya wizi.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana kwa kuwa anafanya kazi katika makao makuu ya wizara jijini Nairobi.

You can share this post!

Waislamu washukuru Saudia kudhamini mahujaji, kupanua...

Juma arejea nyumbani baada ya kutimuliwa Afrika Kusini

adminleo